Categories
Kimataifa

Amnesty International: Uchunguzi ufanywe dhidi ya mauaji ya raia nchini Tanzania

Shirika la kimataifa la Amnesty limewataka maafisa nchini Tanzania kuanzisha uchunguzi huru kuhusu madai ya mauaji na mateso ya wanachama na wafuasi wa mrengo wa upinzani waliokamatwa na kuzuiliwa kiholela kufuatia uchaguzi mkuu wa tarehe-28 mwezi jana.

Mbali na kushinikiza kuachiliwa huru mara moja kwa wale waliokamatwa, mkurugenzi wa shirika la Amnesty International katika kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Deprose Muchena, amesema shirika hilo limefadhaishwa na kukithiri kwa visa vya ukiukaji haki za binadamu baada ya uchaguzi wa urais nchini Tanzania.

Mawakili wa vyama vya upinzani wameliambia shirika la Amnesty International kwamba watu 22 waliuawa na vikosi vya usalama kati ya tarehe ya uchaguzi na tarehe 11 mwezi huu.

Tanzania iliandaa uchaguzi katika mazingira za ukandamizaji na uhasama.

Kabla, wakati na baada ya uchaguzi, vikosi vya usalama vimetumia nguvu kupita kiasi kutawanya mikusanyiko ya amani.

Categories
Kimataifa

Jeshi la Nigeria lakana kuwaua waandamanaji

Jeshi la Nigeria limekanusha madai kuwa liliwaua waandamanaji wasio na silaha kwenye mkutano jijini Lagos mnamo mwezi uliopita.

Wanajeshi hao wamedai kuwa walikuwa wakitumia bunduki ambazo hazikuwa na risasi kwenye makabiliano na raia.

Afisa mmoja mkuu, Brigedia Jenerali Ahmed Taiwo aliwasilisha ushahidi wa kanda ya video kuthibitisha madai yake yaliyotolewa kwa jopo la wachunguzi.

Shirika la Kimataifa la kutetea haki, Amnesty International linasema watu 12 waliuawa wanajeshi walipofyatua risasi wakati wa maandamano ya kupinga ukatili wa polisi katika mtaa wa mabwenyenye wa Lekki, jijini Lagos.

Walioshuhudia waliliambia Shirika la Utangazaji la BBC kuwa wanajeshi waliwafatulia waandamanaji risasi.

Waandamanaji wengine 1,000 walikuwa wamekusanyika kwenye lango la kukusanya ushuru katika barabara ya kueleke mtaa wa Lekki mnamo tarehe 20 Oktoba kuzuia magari kutumia barabara hiyo kuu.

Askari waliripotiwa kuonekana kuweka vizuizi katika barabara ya kuelekea eneo la maandamano muda mfupi kabla ya risasi kuanza kufyatuliwa.

Shambulizi hilo lilitokea baada ya siku kadhaa za maandamano dhidi ya kitengo cha polisi cha Kupambana na Ujambazi, SARS, ambacho mienendo ya maafisa imekashifiwa vikalina na raia wa nchi hiyo.