Categories
Burudani

Likizo ya Mapenzi!

Huu ndio msamiati mpya nchini Tanzania kwa sasa na unatokana na usemi wa mama mzazi wa msanii Ali Kiba.

Mama huyo alikuwa akihojiwa katika kituo cha redio cha Clouds nchini Tanzania ambako alifichua kwamba mke wa Ali kwa jina Amina Khalef yuko nyumbani alikozaliwa Mombasa Kenya kwa ajili ya likizo ya ndoa ama ukipenda mapenzi.

Hili ni dhibitisho kwamba ndoa yao bado ipo kinyume na minong’ono kwamba walisha achana.

Ndoa ya Ali Kiba na mwanadada huyo wa Kenya imekuwa ya misukosuko mingi na mara nyingi huwa inatokea kwamba yuko nyumbani kwao nchini Kenya. Msanii Ali Kiba huwa hapendi kuzungumzia jambo hilo kwenye mahojiano ila analokubali ni kwamba hakuna ndoa ambayo haina matatizo.

Wakati wa mahojiano hayo, mamake Ali Kiba alifichua mengi kuhusu familia yake. Alisema Ali Kiba ndiye kifungua mimba wake na kuna wengine watatu.

Kuna wa pili Abdul kareem ambaye pia ni mwanamuziki kwa jina Abdu Kiba, akifuatiwa na binti wa pekee Zabibu na kitinda mimba ni Abubakar Swadik ambaye ni mpiga picha wa Ali Kiba.

Jina Kiba alisema ni ufupi wa jina “Kibanio” ambalo lilikuwa jina la utani la baba ya watoto wake ila jina halisi la baba Ali Kiba ni “Ng’ang’ise”.

Kulingana naye Ali alianza kuhisi na kupenda muziki akiwa na umri wa siku saba tu. Alipata tatizo mwanzo kukubali kazi ya mwanawe kama mwanamuziki aliyekuwa akiimba nyimbo za kidunia lakini baadaye ilibidi akubali.

Mama Ali Kiba amehudhuria maonyesho yake ya muziki kama mara tatu tu kwa nia ya kujua kinaoendelea humo.

Categories
Burudani

Mwanamuziki wa Tanzania CPwaa aaga Dunia

Mwanamuziki wa nchi ya Tanzania CPwaa ambaye alijulikana sana kwa mitindo kama vile Hip Hop, Rap na Crunk aliaga dunia jana akipokea matibabu katika hospitali ya Muhimbili Jijini Daresalaam.

CPwaa ambaye jina lake halisi ni Ilunga Khalifa anasemekana kuugua ugonjwa wa homa ya mapafu kwa muda.

Mwili wake tayari umezikwa nyumbani kwao katika eneo la Magomeni kulingana na tamaduni za dini ya kiisilamu.

Binamu yake Murad Omar Khamis aliyehojiwa alifichua kwamba Cpwaa amekuwa akiumwa kwa muda wa wiki mbili lakini akazidiwa jumatano na wakamkimbiza hospitali ambapo alilazwa kwenye chumba cha wagonjwa walio hali mahututi.

Alikata roho alfajiri jumapili tarehe 17 mwezi huu wa Januari mwaka 2021.

Wasanii wengi wa Bongo, akiwemo Ali Kiba na TID walifika nyumbani kwa mamake Cpwaa huko Magomeni kwa ajili ya kuifariji familia.

Cpwaa alikuwa akiimba kwenye kundi linalofahamika kama “Park lane” na lilikuwa la watu wawili, yeye na msanii Suma Lee.

Wakiwa pamoja walirekodi na kuzindua vibao kama vile Nafasi nyingine na Aisha lakini kundi hilo baadaye lilisambaratika.

Wasanii wengi na watu maarufu nchini Tanzania walimwomboleza kwenye mitandao ya kijamii kama vile mtayarishaji muziki kwa jina S2kizzy kwenye Instagram. Aliweka picha ya marehemu Cpwaa na kuandika, “RIP big brother Cpwaa. Gone too soon.”

Categories
Burudani

Christine Mosha apatiwa kazi na Sony Music Africa

Mwanadada kwa Jina Christine Mosha maarufu kama “Seven” ambaye hufanya kazi ya kusimamia wasanii kama meneja nchini Tanzania ameteuliwa na kampuni ya kimataifa ya muziki Sony Music Africa kuiwakilisha katika eneo la Afrika Mashariki.

Uteuzi wa Seven ulitangazwa na mkurugenzi mkuu wa Sony Africa Music Sean Watson na kazi yake inaanza mara moja. Watson alimsifia sana Mosha akisema mchango wake kwa Talanta za Tanzania ni mkubwa na kwamba amewahi kushirikiana na Sony Africa kwa njia nyingi.

Majukumu yake yanahusisha kuongoza mauzo ya kampuni hiyo katika eneo la Afrika mashariki, kutafuta na kuandikisha wasanii kwenye kampuni hiyo Afrika mashariki na kusimamia moja kwa moja wasanii hao.

Haya yanajiri siku chache baada ya msanii ambaye amekuwa akisimamia kwa muda Ommy Dimpoz kusajiliwa na kampuni hiyo ya Sony.

Mosha amewahi kufanya kazi na wasanii wengine wengi tajika nchini Tanzania kama vile Rose Muhando, Lady Jaydee, Ali Kiba, Ray C na TID.

Christine Mosha anamiliki kampuni kwa jina “Rockstar 4000 Music Entertainment” ambayo anatumia katika kusimamia wasanii.

Dada Mosha aliwahi kufanya kazi na MTV Africa kati ya mwaka 2005 na mwaka 2010, ambapo mwaka 2006 alikuwa mtangazaji wa kipindi cha “Big Brother Africa.

Akikubali uteuzi huo, Mosha alisema kampuni ya Sony ina wasifu mzuri kimataifa na anashukuru kwa nafasi ya kuonyesha ujuzi wake.

Categories
Burudani

Ni ushauri tu, Baba Levo baada ya kumchamba Harmonize

Mwanamuziki na mtangazaji wa Tanzania Baba Levo anasema kwamba yeye hana ubaya na mwanamuziki Harmonize na kwamba yeye anampa ushauri tu.

Akizungumza wakati akihojiwa, Baba Levo alitoa orodha yake ya wasanii wanne wa kwanza nchini Tanzania. Kulingana naye Diamond Platnumz ni Nambari moja, anafuatiwa na Ali Kiba, wa tatu ni Rayvanny kisha Harmonize anaingia wa nne.

Mtangazaji huyo wa Wasafi Fm alisema kwamba anajaribu tu kumkanya Harmonize aache kung’ang’ana kushindana na Diamond ashindane na Rayvanny ambaye anasema ndiye wa kiwango chake.

Kwenye mahojiano hayo, Baba Levo alifichua kwamba Diamond anamiliki nyumba za kupangisha 126 Jijini Dar Es Salaam pekee.

Harmonize na Diamond awali walikuwa marafiki na yeye ndiye alikuwa msanii wa kwanza kuwahi kusajiliwa na kampuni ya Diamond ya muziki Wasafi Classic Baby (WCB) lakini baadaye akagura na kuanzisha yake kwa jina Konde Music.

Tangu wakati aligura, wengi wanasema kwamba Harmonize anajaribu sana kusababisha ushindani kati yake na Diamond Platnumz.

Diamond naye alisema ushindani ni muhimu katika sekta ya muziki nchini Tanzania lakini hajaonekana kujibu ushindani huo wazi wazi.

Harmonize alitoa wimbo kwa jina “Ushamba” na kwenye video akatumia jamaa mmoja anayefanana sana na Diamond Platnumz na akaima maneno yanayoonekana kumlenga Diamond Platnumz.

Wimbo huo ndio ulisababisha minong’ono ya jinsi Harmonize analazimisha ushindani lakini alijitetea akisema ni burudani tu.

Categories
Burudani

Ommy Dimpoz kujiunga na Sony Music Africa

Mwanamuziki wa nchi ya Tanzania Ommy Dimpoz kwa jina halisi Omary Nyembo atajiunga rasmi na kampuni ya kimataifa ya muziki kwa jina Sony Music Africa kesho.

Habari kuhusu hatua hiyo ya Ommy Dimpoz zilijulikanishwa na meneja wake mmiliki wa kampuni ya muziki nchini Tanzania inayoitwa “Rockstar Africa” mwanadada Seven Mosha.

Mosha aliongeza tena kwamba Ommy Dimpoz atazindua albamu ya kwanza mwakani lakini hivi leo mnamo saa kumi jioni atazindua kibao kipya kwa jina, “Dede”.

Ommy Dimpoz amekuwa kwenye ulingo wa muziki nchini Tanzania kwa muda sasa na anajulikana kwa vibao kama vile, “Tupogo”, “Nai Nai” na vingine.

Alianza kuimba mwaka 2005 akiwa shule ya upili pale alipoanzisha kundi kwa jina “West VIP”. Aliimba pia katika kundi jingine kwa jina “Top Band” hadi mwaka 2011 alipoamua kuimba peke yake.

Wimbo wake wa kwanza ‘Nai Nai’ uliwahi kuteuliwa na kushinda kwenye tuzo kadhaa hata zile za Kenya kwa jina ‘Nzumari”.

Ameshirikisha wanamuziki wengine tajika katika kazi yake kama vile Christian Bella, Dully Sykes na Avril wa Kenya kati ya wengine wengi.

Mwaka 2018 afya yake ilidhoofika ikasemekana kwamba alikuwa anaugua saratani akaja Kenya kutafuta matibabu kisha akaelekezwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.

Alipohojiwa baada ya kupona, alisema kwamba Gavana wa kaunti ya Mombasa Hassan Joho aligharamia kikamilifu matibabu yake.

Mwanamuziki wa Tanzania Ali Kiba pia yuko chini ya hiyo lebo ya kimataifa ya Sony.

Categories
Burudani

Nandy akiri kuandikiwa wimbo

Mwanadada Nandy ana kibao kipya kwa jina “Nibakishie” ambacho amemshirikisha Ali Kiba ambaye amekuwa kwenye ulingo wa muziki nchini Tanzania kwa muda mrefu.

Wimbo huo ni wa mapenzi na wawili hao wanaonyeshana mapenzi kwenye video ya wimbo wao mpya ambayo ni ya uzuri wa hali ya juu.

Wawili hao kwanza walizindua sauti ya wimbo pekee kwenye majukwaa kadhaa ya muziki mitandaoni ambapo ulisikilizwa kwa wingi na baadaye wakaweka video yake kwenye youtube ambapo pia kufikia sasa umetazamwa zaidi ya mara laki sita.

Binti huyo ambaye pia hujiita “The African Princess” amemshukuru mwanamuziki na mwandishi wa nyimbo kwa jina “Kusah” kwa kumwandikia wimbo huo. Kulingana naye, wimbo huo umemletea mafanikio mengi hadi sasa.

Alisema hakuna ubaya kwa mwanamuziki aliyeendelea kuandikiwa nyimbo kwani waandishi wa nyimbo pia wanahitaji kupata riziki.

Aliwaalika waandishi wengine wa nyimbo ambao wana kazi ambazo wanaonelea zitamfaa kwamba yuko tayari kwa biashara. Haijulikani kama Kusah aliandika maneno yote ya wimbo huo hata sehemu ambayo inaimbwa na Ali kiba.

Nandy amekuwa pia akionyesha picha za matukio wakati wakirekodi video ya wimbo huo na kwa wakati mmoja anakaribia kulia kwa woga kwamba angezama majini kwenye kidimbwo kimoja ambapo walikuwa.

Wanamuziki wenza wamempongeza kwa kazi hiyo huku wakimtania kama vile Ommy Dimpoz ambaye aliweka sehemu ya video ya wimbo huo kwenye Instagram na kuandika,

“Sema Hakuna mtu Mvumilivu na Mwenye Moyo Wa Chuma Kama billnass. Ndo Maisha kaka uzuri ulikuwepo location. Anyway tuendelee kuenjoy mziki mzuri kutoka kwa officialalikiba na officialnandy. Nibakishie. link on their bio”

Alikuwa akimtania mpenzi wa Nandy kwa jina Billnass ambaye pia ni mwanamuziki. Wema Sepetu ambaye ni muigizaji aliandika, “yaani nyie mngekuwa wapenzi, nasema tu.” kwenye picha ya Nandy na Ali Kiba.

Categories
Burudani

Tanasha Donna kuzindua Albamu yake mwakani

Mamake Naseeb Junior Tanasha Donna ametangaza kwamba mwaka ujao atazindua albamu yake ya kwanza.

Bi Donna ambaye pia aliwahi kuwa mtangazaji wa redio, alisema hayo kupitia Instagram ambapo aliandika,

“Mwaka 2020 umekuwa mwaka wa vibao moto.

Vibao saba kwa muda wa chini ya mwaka mmoja, na sio mimi, ni kwa sababu ya upendo na usaidizi ambao mmeendelea kunionyesha. Alhamdulillah. Mwaka 2021 tunaangusha albamu. Albamu yetu. Tuweke historia. Afrika mashariki kwa ulimwengu.”

Mwanzo wa mwaka huu, Tanasha alizindua ‘EP’ yaani “extended play” yake ya kwanza kwa jina “Donnatella” ambayo ilipokelewa vyema na mashabiki.

Kwenye mkusanyiko huo wa nyimbo kuna nyimbo kama vile ‘Gere’ ambao alishirikiana na aliyekuwa mpenzi wake Diamond Platinumz ambaye pia ni baba ya mtoto wake. Wimbo kwa jina ‘La Vie’ ambao amemshirikisha mwanamuziki wa Tanzania Mbosso ambaye yuko chini ya kampuni ya Wasafi inayomilikiwa na Diamond. Na wimbo ‘Sawa’ kati ya nyingine.

“EP” au Extended Play katika muziki ni mkusanyiko wa nyimbo ambao hautoshi idadi ya kuitwa albamu. Mama huyo wa mtoto mmoja wakati fulani alisemekana kudandia umaarufu wa mpenzi wake wa awali Diamond ili kuendeleza muziki wake.

Tanasha alikiri kwamba uhusiano wake na Diamond ulisaidia kuinua kazi yake lakini hata yeye ametia bidii kwenye fani hiyo. Tanasha pia ni mwanamitindo na aliwahi kufanya kazi na mwanamuziki Ali Kiba wa Tanzania ambaye huchukuliwa kuwa hasidi wa Diamond hata kabla ya uhusiano wake na Diamond.

Binti huyo alionekana kwenye video ya wimbo ‘Nagharamia’ wake Ali Kiba akiwa amemshirikisha Christian Bella.

Categories
Burudani

Video ya “Ushamba” wimbo wa Konde Boy

Harmonize aliutambulisha wimbo huo rasmi usiku wa tarehe mosi mwezi huu wa Novemba wakati wa tamasha la “Ushamba Night Party” ila kwa wakati huo ulikuwa ni sauti tu na jana tarehe nane mwezi Novemba ameachia video ya wimbo huo.

Maneno ya wimbo huo kwenye ubeti wa pili yanaonekana kuingilia anaoshindana nao katika ulingo wa muziki nchini Tanzania na kwenye video inadhihirika wazi kwamba anayemzungumzia ni Simba au ukipenda Diamond Platinumz.

Amemtumia jamaa fulani ambaye anafanana na Diamond Platinumz ambaye hujiita “Diamond wa Buza” kwenye video katika sehemu ya wimbo ambayo inazungumzia Simba. Ni katika ubeti huo wa pili na maneno ni ” … Halina meno hilo simba likila demu lazima litangaze …”.

Diamond wa Buza anaonekana akiwa kwenye kidimbwi cha kuogelea akiwa na mwanadada na wanapiga picha, taswira ya matukio yaliyozua minong’ono kwenye mitandao ya kijamii wakati ambapo Diamond Platinumz alionekana akiogelea nyumbani kwake na mwanamuziki Mimi Mars.

Hayo yalifanyika siku chache baada ya Diamond Platinumz kukiri kwamba anampenda dada huyo wa mwanamuziki Vanessa Mdee.

Harmonize amefuata nyayo za Ali Kiba kwa kutoa wimbo wa kukejeli washindani baada yake kutoa wimbo kwa jina “Mediocre” na tafsiri yake ni “ujinga”. Hata hivyo Ali Kiba alikana tetesi kwamba wimbo huo ulilenga washindani wake ambao ni Diamond na Harmonize.

Diamond kwa upande mwingine anaonekana kuridhika na ushindani huo katika ulingo wa muziki maanake alipohojiwa katika kituo chake cha redio “Wasafi Fm” tarehe 27 mwezi Oktoba mwaka huu alisema ushindani huo ni muhimu unafanya fani iendelee.

Wasafi news pia asubuhi ya leo wameandika wakisema Harmonize anamlenga bosi wake wa zamani ambaye ni Diamond Platinumz. Harmonize aligura WCB kampuni ya muziki ya Diamond Platinumz ila hajakamilisha taratibu za kujiondoa kabisa.

Tazama video ya wimbo Ushamba hapa chini;

Categories
Burudani

Ushindani lazima uwepo, Diamond Platinumz

Mwanamuziki tjika nchini Tanzania, Afrika mashariki, Afrika na hata ulimwenguni Diamond platinumz ameashiria kwamba kule kutopatana au ushindani kati yake na wanamuziki wengine kama vile Ali Kiba kutaendelea kuwepo.

Simba huyo wa muziki nchini Tanzania aliyasema hayo wakati akihojiwa kwenye kipindi kiitwacho “The Switch” cha kituo cha redio cha Wasafi ambacho anamiliki.

Kulingana naye zogo kidogo ni ladha katika ulingo wa muziki ila lisichukuliwe kibinafsi kiasi cha wengine kutaka kudhuru wengine.

” Ni kama sasa tuseme timu ya soka ya Simba iungane na timu ya Yanga, hiyo itakuwa nini sasa? Ndio mpira utakuwa umekufa kabisa.” alisema Diamond.

Msanii huyo anasema lazima ushindani uonekane hasa kwa ubunifu ndio wasanii wajikaze na sanaa iendelee mbele lakini akahimiza kwamba mashindano kama hayo yawe chanya.

“Kwa ukweli vitu kama hivyo lazima viwepo ila watu wasivichukulie kuwa personal watu wasiviingize kwa familia zao, waanze kurogana wataharibu hii sanaa.” alielezea Diamond.

Rais John Pombe Magufuli kwenye Kampeni za kutafuta kuchaguliwa tena kupitia chama cha CCM aliwaleta pamoja Ali Kiba, Diamond na Konde Boy almaarufu Harmonize.

Diamond alifichua pia kwamba ametambuliwa kwa mchango wake katika sekta ya burudani na jamii kwa ujumla nchini Tanzania ambapo mwaka 2018 aliambiwa achague mtaa nyumbani kwao ambao utabadilishwa jina na kuitwa jina lake.

Hadi sasa hajachagua mtaa.

jambo lingine ambalo Diamond ameliweka wazi siku za hivi karibuni ni jengo ambalo litakuwa afisi za Wasafi Media ambalo alisema ujenzi wake unakaribia kukamilika.

Jumba hilo “Wasafi Towers” linasemekana kuwa katikati ya mji wa Dar Es Salaam na litakuwa nyumbani kwa kampuni ya muziki ya Wasafi almaarufu WCB, kituo cha runinga na kile cha redio vyote ambavyo viko chini ya Wasafi Media.

Categories
Kimataifa

Wanamuziki kwenye Kampeni nchini Tanzania

Yeyote ambaye amekuwa akifuatilia kampeni za uchaguzi mkuu wa leo eneo la Zanzibar na Kesho katika eneo zima la Tanzania atakubaliana na kauli kwamba wanamuziki wamehusika sana.

Swali ambalo linachipuza sasa ni hili, kwa nini wamejiingiza vile kwenye siasa? Muziki au nyimbo nchini Tanzania ni kitu ambacho huchukuliwa kwa uzito mkubwa.

Vizazi vyote nchini humo vinapenda muziki wa aina fulani na raia nchini humo wanawaenzi na kuwafuatilia kwa karibu wasanii hasa kwenye mtandao wa Instagram ambao ni maarufu sana nchini Tanzania.

Huenda wasimamizi wa mipango katika vyama vya kisiasa walionelea wanamuziki kuwa nguzo muhimu katika kuvutia watu wengi kuhudhuria mikutano ya kampeni.

Wengi wa wasanii ukizingatia mitindo tofauti ya nyimbo, waliandaa nyimbo za kusifia wanasiasa na vyama vya kisiasa kulingana na sehemu ambayo wanaunga mkono.

Bi. Zuchu ambaye ni kitinda mimba wa sasa wa kampuni ya muziki ya Wasafi inayomilikiwa na Diamond Platinumz hajaachwa nyuma kwani ana wimbo wa mtindo wa raggae ambao yeye huimba kila akiwa kwenye kampeni za chama tawala cha CCM ambacho wasanii wengi wanaunga mkono.

Mkubwa wake Diamond alibadilisha kidogo maneno kwenye wimbo wake maarufu wa ‘baba lao’ ambapo anarejelea mgombea urais wa CCM Rais Magufuli kama baba lao na pia alibadilisha maneno ya wimbo ‘number one’ akaunda wimbo kwa jina ‘CCM number one’.

Harmonize ambaye aligura Wasafi na kuanzisha ‘Konde Music’ alibadilisha maneno kwenye wimbo wa ‘Kwangwaru’ akaweka maneno ya kusifia utendakazi wa Rais John pombe Magufuli na chama cha CCM. Mwanamuziki huyo ambaye siku hizi anajiita mjeshi ana wimbo mwingine pia wa kusifia CCM kwa jina CC.

Ni baadhi tu ya nyimbo ambazo zimeimbwa na wasanii wa Tanzania katika kuunga mkono chama tawala cha CCM ila ni wengi ambao huwa wanahudhuria mikutano ya chama hicho na kukipigia debe.

Wengine ambao huenda kutumbuiza kwenye mikutano ya CCM ni kama vile Ali Kiba na wengine kutoka kwa kampuni yake ya muziki ya ‘king’s music’, Shilole, Nandy na wengine wengi ambao ni wasanii huru na wa kampuni ya Wasafi.

Kunao wengine ambao wamechagua kuunga mkono vyama vya upinzani kama vile Roma Mkatoliki na Ney wa Mitego.

Mhadhiri wa chuo kimoja kikuu nchini Tanzania Dakta Viscencia Shule alizungumza na BBC ambapo alielezea kwamba mara nyingi utakuta wanamuziki hawajiingizi kwa kampeni kwa hiari ni vile inabidi.

Kulingana naye serikali ya Tanzania iliweka sheria kali za kudhibiti maadili katika sekta ya burudani ambazo zimewagusa wasanii kwa njia moja ama nyingine.

Wengi wameadhibiwa na Baraza La Sanaa La Taifa almaarufu BASATA kwa nyimbo au vitendo ambavyo vinaonekana kukiuka maadili na hivyo lazima wajiweke upande wa serikali wasionekane waasi.