Categories
Habari

Muda wa kutafuta paspoti ya kisasa waongezwa hadi mwezi Disemba mwaka huu

Serikali kupitia idara ya uhamiaji imeongeza kwa miezi kumi zaidi hadi tarehe 31 Disemba mwaka huu muda wa kutafuta paspoti ya kisasa.

Haya yanajiri huku idara ya huduma za uhamiaji ikipunguza shughuli zake katika juhudi za kukabiliana na msambao wa ugonjwa wa COVID-19 hapa nchini.

Kwenye taarifa iliyotolewa kwa vituo vya habari na waziri wa usalama wa kitaifa Dkt. Fred Matiang’i, muda huo unaongezwa kwa mara ya mwisho baada ya muda kuongezwa kwa mara ya kwanza mwezi Februari mwaka uliopita.

Waziri ametoa wito kwa wakenya kufanya mipango ya kupata paspoti hiyo ya kielektroniki ili kuepusha matatizo yanayotokana na shughuli za usafiri wa kutafuta stakabadhi hiyo huku serikali ikijaribu kuondoa paspoti ya zamani na kuanzisha utumiaji wa paspoti mpya ya jumuia ya Afrika Mashariki .

Serikali imesema kuanzia tarehe Mosi Januari mwaka ujao paspoti ya zamani haitakubalika tena.

Categories
Habari

Wabunge washinikiza kuimarishwa kwa biashara kati ya Kenya na Tanzania

Kamati ya Bunge kuhusu Ushirikiano wa Kanda ya Afrika Mashariki imeweka mikakati ya kuimarisha biashara kati ya Kenya na Tanzania.

Akiongea wakati wa ziara mjini Isebania, Naibu Mwenyekiti wa kamati hiyo Ruweida Mohamed amesema biashara kupitia mpaka wa Kenya na Tanzania imekumbwa na changamoto ambazo zimeathiri mazingira ya utendaji biashara baina ya mataifa husika.

Hata hivyo, Ruweida ameeleza kuridhika na upimaji wa ugonjwa wa Korona kwenye mpaka huo ambao umeimarika kwa kiasi kikubwa licha ya changamoto za kisera kwenye mataifa husika.

Aidha ameeleza kufadhaishwa na ukosefu wa ushirikiano kati ya serikali ya taifa na ile ya Kaunti.

Wafanyabiashara wa humu nchini walikuwa wanalalamikia kuhangaishwa na maafisa wa usalama wa Tanzania na kufutiliwa mbali kwa leseni zao za kuhudumu.

Awali, katibu katika idara ya jumuiya ya Afrika Mashariki Kevit Desai, alisema serikali imejitolea kuwakinga wafanyabiashara dhidi ya athari za ushuru wa juu.

Categories
Habari

Madereva wa malori wataka muda wa matumizi ya vyeti vya Corona uongezwe

Madereva wa malori ya safari ndefu wanaomba Wizara ya Afya kufanyia marekebisho masharti ya kupimwa virusi vya Corona kila baada ya siku 14.

Madereva hao wanadai kwamba hitaji hilo haliwezi kutekelezwa kwani inawachukua siku hizo 14 kusafiri kutoka bandari ya Mombasa kwenda maeneo kadhaa ya kanda ya Afrika Mashariki.

Madereva waliozungumza katika mji wa mpakani wa Malaba ulioko Kaunti ya Busia wanasema kipindi hicho cha wiki mbili kinawagharimu zaidi kwani wengi wao hutumia hata zaidi ya siku 14 kusafiri kati ya Mombasa na mataifa mengine ya kanda hii.

Mmoja wa madereva hao, Alex Wambua, amesema vyeti vyao vya kuthibitisha hali yao ya kiafya hufikia muda wa mwisho kabla ya kurejea nchini kwa hivyo wanalazimika kutumia kiasi cha shilingi 7,000 za Kenya ili kupimwa virusi hivyo nchini Sudan Kusini na Uganda.

“Wiki mbili ni muda mfupi sana. Tunaomba serikali ya Kenya ilete mfumo ambapo madereva wanapimwa kila baada ya siku 30 badala ya siku 14 kwa sababu baadhi yetu tunatumia muda huo wa siku 14 kusafiri hadi Kampala, Kigali au Juba,” akasema Wambua.

Dereva mwingine, Seneta Mwashumba, ambaye alikuwa akielekea Juba, anasema msongamano wa magari katika mji huo wa mpakani bado ni shida hata baada ya kuanzishwa mfumo wa madereva kupimwa kabla ya kuanza safari.

Mwashumba anadai kwamba wanazuiiwa kwenye mpaka wa Malaba kwa siku tatu zaidi.

“Kwa mfano mimi tayari nimepimwa, niko na cheti na lori langu limeidhinishwa kusafiri. Lakini sijaweza kuanza safari na nimekwama hapa kwa siku tatu,” akasema.

Madereva wengine wanasemekana kutumia siku 11 kati ya Mombasa na Bungoma kabla ya kujiunga na foleni mpakani ambapo wanapaswa kutumia siku nyingine nne na kulazimika kupimwa tena baada ya kukamilika kwa siku 14.

Categories
Habari

Waziri Amina aungwa mkono Afrika Mashariki kwa cheo cha WTO

Jamii ya Afrika Mashariki imemuunga mkono Waziri wa Michezo humu nchini Balozi Amina Mohammed anayewania nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani, WTO, kufuatia ombi la Rais wa Rwanda Paul Kagame.

Kwenye barua iliyotumwa kwa Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Adan Mohammed na wenzake wa Rwanda, Burundi, Uganda na Tanzania, Mwenyekiti wa Baraza la Afrika Mashariki Vincent Biruta amesifu mataifa ya jumuiya hiyo kwa kukubali kumuunga mkono mgombea Amina Mohammed.

“Nakujulisha kwamba Balozi Amina Mohammed ameungwa mkono kama mgombea wa Jamii ya Afrika Mashariki katika kuwania nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani,” akasema.

Haya yanajiri huku awamu ya pili ya mashauri kuhusu kumchagua Mkurugenzi Mkuu mpya wa shirika hilo ikifika tamati.

Lengo la mashauri hayo ni kupunguza wagombea waliosalia kutoka watano hadi wawili.

Waziri Amina amekiri kufurahishwa na uungwaji mkono huo.

“Nawashukuru Mawaziri wa Biashara wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuunga mkono azma yangu ya kuwa Mkurugenzi Mkuu mpya wa Shirika la Biashara Ulimwenguni,” amesema Balozi Amina.

Ameahidi kutumia tajriba yake ya maswala ya biashara na siasa na kuchukua jukumu la kibinafsi kuanzisha mchakato wa mashauri kuhusu mageuzi ya shirika hilo.

“Iwapo nitashinda, nitatumia nguvu zangu zote, ujuzi, elimu na tajriba yangu katika kutekeleza majukumu haya. Kutokana na uzoefu wa kuwa waziri kwa muda mrefu na kuhusika katika mazungumzo ya kimaeneo na kimataifa, nimetayarika kwa majukumu haya,” akaongeza.

Aidha, Amina ameahidi kusaidia mataifa ya Afrika Mashariki kukamilisha mazungumzo kuhusu ruzuku ya sekta ya uvuvi na kilimo.