Timu ya taifa ya Ghana maarufu kama Black satelites ndio mabingwa wa makala ya 16 ya kombe la bara Afrika kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 baada ya kucharaza Uganda Hippos magoli 2-0 kweny fainali iliyosakatwa uwanjani Olympic mjini Noukchott Mauritania Jumamosi usiku.
Uganda Hippos waliokuwa wakishiriki michuano hiyo kwa ra ya kwanza walianza kwa utepetevu na kukosa maarifa na kumruhusu nahodha Daniel Afriye kuiweka Ghana uongozini katika dakika ya 22 akiunganisha pasi yake Fattaw Issakhu na kuongoza hadi mapumzikoni.
Waganda walijaribu kurejea mchezoni lakini kosa la mabeki dakika ya 51 likampa Afriye fursa ya kutanua uongozi wa Ghana kwa goli la pili matokeo yaliyodumu hadi kipenga cha mwisho.
Mshambulizi wa Uganda Derrick Kakooza aliibuka mfungaji bora kwa magoli 5 huku kocha Morley Byekwaso akitawazwa kocha bora wa mashindano hayo.
Ilikuwa mara ya kwanza kwa Ghana kunyakua kombe hilo tangu mwaka 2009 na kusawazisha rekodi ya Black Stars ambayo pia imetwaa kombe la Afrika mara 4.