Categories
Kimataifa

Umoja wa Mataifa waonya kuzuka kwa mzozo wa kibinadamu katika jimbo la Tigray

Umoja wa mataifa umeonya kwamba mzozo mkubwa wa binadamu unanukia katika jimbo la Kaskazini mwa Ethiopia la Tigray,kufuatia mapigano ya wiki mbili katika eneo hilo.

Umoja huo umesema takriban watu elfu-27 tayari wamehamia nchi jirani ya Sudan na kwamba wafanyakazi wake nchini humo wanakabiliwa na changamoto kuhudumia idadi inayongezeka ya wanaohitaji msaada.

Mapigano hayo yalizuka baada ya serikali ya Ethiopia kuwashutumu  wapiganaji wa Tigray,kwa uhaini.

Duru zinaarifu kuwa mamia ya watu wameuawa kwenye mapigano hayo,ingawaje idadi kamili haijabainishwa.

Nchi jirani za Kenya na Uganda zimetoa wito wa kufanywa mazungumuzo kurejesha utulivu katika eneo hilo.

Kwenye ujumbe wake kwa njia ya mtandao wa kijamii wa Twitter, Rais Uhuru Kenyatta alitahadharisha kuhusu athari za mzozo huo kwa nchi hizi mbili.

Serikali ya Ethiopia hata hivyo imeondolea mbali uwezekano wa kufanya mashauri na kundi hilo,ambalo inasema lengo lake ni kuleta vurugu nchini humo.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alinukuliwa akisema  oparesheni ya kijeshi katika jimbo la Tigray imo katika hatua ya mwisho.

Categories
Habari

Rais Kenyatta ataka mazungumzo ya amani kukomesha mzozo nchini Ethiopia

Rais Uhuru Kenyatta amejiunga na viongozi wengine wa kimataifa kutaka mapigano kaskazini mwa Ethiopia yakomeshwe kupitia njia ya mazungumzo.

Kwenye ujumbe wake kwa njia ya mtandao wa kijamii wa Twitter, Rais Kenyatta ametahadharisha kuhusu athari za mzozo huo kwa nchi hizi mbili, ambazo zimekuwa wasuluhishi wa mizozo katika kanda hii navielelezo vya amani na uthabiti

Rais alisema hayo baada ya kukutana na Naibu Waziri Mkuu wa Ethiopia, aliye pia Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi hiyo Demeke Mekonen katika Ikulu ya Nairobi.

Mekomen pia alimpa Rais Kenyatta ujumbe maalum kutoka kwa Waziri Mkuu wa Ethoipia Abiy Ahmed kuhusu maswala mbali mbali ikiwemo hali ya siasa na usalama Ethiopia.

Kwenye mkutano huo, Rais Kenyatta alikuwa ameandamana na Waziri wa Mashauri ya Kigeni humu nchini Raychelle Omamo, Katibu wake Ababu Namwamba na Mkuu wa Utumishi wa Umma Dkt. Joseph Kinyua.

Viongozi kadhaa wa kimataifa wamewataka wapiganaji wa kundi la TPLF kusitisha  mapigano ambayo yanavuruga mafanikio yaliyokuwa yamepatikana na kutatiza juhudi za Ethiopia za kustawisha nchi hiyo.

Categories
Kimataifa

Mulu Nega ateuliwa kuwa msimamizi mkuu wa jimbo Tigray.

Serikali ya Ethiopia imemteua msimamizi wa muda wa jimbo la Tigray kaskazini ya nchi hiyo ambako operesheni ya kijeshi ya kuwang’atua watawala.

Taarifa fupi iliyotolewa na waziri mkuu Abiy Ahmed ilisema kuwa Dkt. Mulu Nega ameteuliwa kuwa msimamizi mkuu wa jimbo hilo.

Ilisema kuwa afisa huyo mkuu atasajili na kuteua wakuu wa asasi kuu za kiserikali wa jimbo hilo kutoka kwa vyama vya kisiasa vinavyotekeleza shughuli zao kwa njia halali katika eneo hilo.

Hapo awali, wabunge walikuwa wamepitisha azimio la kuanzisha utawala wa mpito kuwajibika kwa serikali ya shirikisho katika jimbo la Tigray.

Uteuzi huo unaonyesha azma ya Abiy ya kumuondoa anayesimamia Ukombozi wa Watu wa Tigray  kutoka kwa mamlaka.

Siku ya Alhamisi, bunge la kitaifa lilimwondolea gavana wa Tigray kinga dhidi ya mashtaka.

Categories
Kimataifa

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed awatimua maafisa wakuu Serikalini

Waziri mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, amemfuta kazi mkuu wa majeshi, mkuu wa idara ya ujasusi na waziri wa mashauri ya kigeni.

Hatua hiyo inajiri huku jeshi likiendelea na mashambulizi kwa siku ya tano katika eneo linalokumbwa na ghasia la Tigray kwa kutekeleza mashambulizi mapya ya angani.

Afisi ya Abiy ilitangaza mabadiliko hayo kupitia mtandao wake wa Twitter, bila kutoa sababu zozote kwa mabadiliko hayo yaliofanywa.

Abiy anaendelea na kampeni yake ya kijeshi aliotangaza siku ya Jumatano licha ya miito ya kimataifa ya kutaka mashauri kufanywa na kundi la Tigray People’s Liberation Front (TPLF).

Raia wa Tigray walithibiti siasa za Ethiopia kwa miongo kadhaa hadi Abiy alipochukua hatamu za uongozi mwaka wa 2018 na wanapigana kupinga juhudi zake za kupunguza ushawishi wao mkubwa.

Ofisi ya Abiy ilisema naibu waziri mkuu,Demeke Mekonnen, ameteuliwa kuwa waziri wa mashauri ya kigeni na Birhanu Jula amepandishwa cheo kuwa mkuu wa majeshi kutoka kwa cheo chake cha awali cha naibu mkuu wa majeshi.

Abiy pia amemteua Temesgen Tiruneh ambaye alikuwa rais wa eneo la Amhara, kuwa mkuu mpya wa idara ya ujasusi.

Watu milioni nne wamo hatarini ya kuachwa bila makazi kutokana na zogo lineloongezeka katika eneo la Tigray nchini Ethiopia kwa mujibu wa ripoti ya umoja wa mataifa.

Categories
Kimataifa

Addis Ababa yashtumu matamshi ya Washington dhidi ya bwawa tata la Nile

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed  amesema kuwa taifa lake halita-itikia shinikizo zozote hasa baada ya rais wa Marekani  Donald Trump kupendekeza kuwa huenda Misri ikaharibu bwawa tata la Nile.

Bwawa hilo la the Grand Ethiopian Renaissance linazozaniwa na mataifa ya  Ethiopia, Misri na  Sudan.

Trump alisema kuwa Misri huenda isiweze kuishi na bwawa hilo na huenda ikalilipua.

Hata hivyo Ethiopia inaamini kuwa Marekani inaiunga mkono Misri katika mzozo huo.

Marekani ilitangaza mwezi Septemba kuwa itakatiza misaada kwa  Ethiopia baada yake kuanza kujaza eneo moja lililo nyuma ya bwawa hilo mwezi Julai.

Misri inategemea zaidi  mto Nile kwa mahitaji yake mengi ya maji na inahofia kuwa huenda huduma hizi zikakatizwa na uchumi wake kuathirika iwapo  Ethiopia itatwaa udhibiti wa mto huo.

Pindi baada ya kukamilika, bwawa hilo la gharama ya dola bilioni 4 katika eneo la  Blue Nile magharibi mwa Ethiopia litakuwa mradi mkubwa zaidi wa kuzalisha kawi kutoka kwa maji barani Afrika.

Ujenzi wa bwawa hilo ulianza mwaka 2011 huku kitendawili kikuu kikiwa muda utakaotumiwa kujaza bwawa hilo.