Stevie Wonder kuhamia Ghana

Mwanamuziki nguli wa Marekani Stevie Wonder ameamua kwamba atahamia nchini Ghana barani Afrika kabisa.

Wonder alirudia kutangaza nia ya kuhamia Ghana kwenye mahojiano na Oprah Winfrey. Alikuwa akizungumzia taifa la Marekani kabla ya uchaguzi wa mwaka jana ambapo aliahidi kwapa wamarekani wimbo wa mwisho kabla ya kuhamia Ghana.

Wakati huo, Stevie alihisi kwamba mambo mengi yalikuwa yamekwenda visivyo nchini Marekani na nchi hiyo inahitaji miaka kama mitano ili kurekebisha hali.

Mara ya kwanza mwanamuziki huyo asiye na uwezo wa kuona kutangaza kwamba angehamia Ghana ni mwaka 1994 na alisema alivutiwa na taifa hilo la kiafrika baada ya kulizuru mara kadhaa.

Sababu kuu ya mwanamuziki huyo kuhama Marekani hata baada ya kuwa na wakati mwema kwenye ulingo wa muziki kwa miaka kadhaa ni heshima kwake na kwa watu wa ukoo wake.

Stevie hataki watoto wake na watoto wa watoto wake wawe wakiomba kuheshimika na kupendwa kwenye mazingira yao ya kila siku yaani hataki wabaguliwe na kujihisi kwamba hawatoshi na kwamba wao sio wa maana.

Wonder wa miaka 70 sasa, na baba wa watoto 9, amechoshwa na hatua ya Marekani kukosa kuthamini raia wake wote kwa njia sawa

Taifa la Ghana limekuwa likikaribisha wahamiaji kama hao kutoka Marekani na limewatengea ardhi ya kujenga makazi yao.

Hata hivyo wahamiaji hawaruhusiwi kununua kabisa ardhi nchini Ghana ila wanaikodisha kutoka kwa serokali kwa muda wa miaka 50.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *