Stars kucheza mechi tatu za kujipiga msasa kabla ya kuikabili Misri

Timu ya taifa Harambee Stars imeratibiwa kucheza mechi tatu za kirafiki kunoa makali kabla ya kukabiliana na Misri katika pambo la kundi G kufuzu dimba la Afcon tarehe 22 mwezi ujao katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani.

Stars watapambana na Sudan Kusini tarehe 13 mwezi ujao hapa Nairobi ,kabla ya kuwaalika Tanzania siku mbili baadae na kuzuru Tanzania tarehe 18 .

Kenya itawaalika Pharoes ya Misri katika pambano la tano kundi G Machi 22 kabla ya kusafiri kwenda Lome Togo kwa mkwangurano wa mwisho tarehe 30 mwezi ujao.

Mechi hizo zitakuwa za kuhitimisha tu ratiba kwa Kenya ambayo haina fursa ya kuzipiku Misri na Comoros zilizo kileleni pa kundi hilo, ili kufuzu kwenda AFCON kwa mara ya pili mtawalia kwa mara ya kwanza ,baada ya kushiriki mwaka 2019 nchini Misri.

Comoros inaongoza kund F kwa pointi 8 sawia na Misri huku timu hizo mbili zikimenyana katika mchuano wa mwisho tarehe 30 mjini Cairo Misri ,mataifa yote yakihitaji kwenda sare ili kutwaa nafasi hizo mbili.

Kabla ya hapo Comoros watakuwa na fursa ya kufuzu watakapowaalika Togo tarehe 22 mwezi Machi wakiwania tu sare ili kujikatia tiketi kwa mara ya kwanza.

Kenya ni ya tatu kundini G kwa alama 3 wakati Togo ikiwa imezoa pointi 1.

Wakati uo huo wachezaji 28 wa humu nchini wameitwa kambini kujiandaa kwa mtihani huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *