Sossion alaumiwa kwa kusambaratisha chama cha walimu cha KNUT

katibu Mkuu wa chama cha walimu humu nchini-KNUT  Wilson Sossion, sasa anakabiliwa na uasi katika chama hicho huku maafisa kutoka maeneo ya Nyanza, Rift Valley na magharibi wakiazimia kumng’atua katika uchaguzi unaotarajiwa kuandaliwa mwezi machi mwaka huu.

Wakiongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho katika eneo la  Nyanza Tobias Ogalo, maafisa hao walisema kuwa  Sossion amesambaratisha matawi yote  110 ya chama hicho cha KNUT kote nchini.

Hali hiyo wanasema imesababisha ukosefu wa fedha, huku maafisa katika matawi hayo na wafanyikazi wakikosa kulipwa kwa muda wa miezi 18 iliyopita.

Ogalo alimshauri Sossion kuchagua baina ya kuhudumu wadhifa wa katibu mkuu wa chama cha  walimu cha KNUT au kuwa mbunge maalum.

Katibu Mkuu wa chama cha walimu cha KNUT katika kaunti ya Migori Caleb Opondi, alimshtumu Sossion kwa kukosa kuwakilisha ipasavyo walimu kutokana na uhusiano mbaya na tume ya kuwaajiri walimu nchini-TSC.

Matamshi sawa na hayo yalitolewa na katibu mkuu wa chama cha KNUT kaunti ya Kericho  Stanley Mutai ambaye alisema kuwa mbunge huyo maalum anapaswa kujianda kuondoka katika uongozi wa chama hicho.

Maafisa hao walikuwa wakiwahutubia wanahabari huko  Sondu baada ya kufanya mkutano wa faraghani. Juhudi za kupata maoni ya Sossion hazikufua dafu.

Uchaguzi huo awali ulikuwa umepangwa kufanyika tarehe 4 mwezi huu lakini tarehe hiyo ikawiana na siku ya ufunguzi wa shule.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *