Sonko afikishwa mahakamani Kiambu na kukanusha mashtaka ya kuzua vurugu

Aliyekuwa Gavana wa Kaunti ya Nairobi Mike Sonko amefikishwa katika Mahakama ya Kiambu ambapo amekanusha mashtaka kadhaa dhidi yake yanayohusiana na vurugu.

Baada ya kulala korokoroni usiku wa kuamkia Jumanne, Sonko amefikishwa katika mahakama hiyo alikosomewa mashtaka yanayomkabili.

Mashtaka hayo yanahusiana na kisa ambapo anasemekana kuongoza kundi lililowashambulia watu kadhaa katika eneo la Buruburu Phase 4, huko Kamukunji, Kaunti ya Nairobi.

Inadaiwa kwamba mnamo tarehe 25 mwezi Mei mwaka wa 2019, kundi hilo, likiongozwa na Sonko, liliingia kwa lazima katika ardhi ya Kampuni ya Landmark International Properties na kuwajeruhi Evans Obaga, George Chege, Paul Kahiga na Charles Karori, Alex Kioko, Stephen Ouma, Musyoki Kavunda, John Mungai Wanjiru na Joel Kinja Muthui.

Hata hivyo Sonko amekana madai yote dhidi yake, huku Wakili wake akiwasilisha ombi la kumtaka mteja wake aachiliwe kwa dhamana.

Sonko alihojiwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Uhalifu (DCI) siku ya Jumatatu baada ya kutii mwito wa idara hiyo wa kumtaka afike mbele yake.

Sonko amepitia masaibu mengi ikiwemo kubanduliwa mamlakani mnamo mwezi Desemba mwaka uliopita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *