Sisi ndio kusema, EACC yaonya kuhusu maadili ya wanaotaka kuwania nyadhifa serikalini

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi nchini (EACC) imeonya kwamba mtu yeyote anayeta kuwania wadhifa kwenye uchaguzi sharti apate idhini ya tume hiyo kabla ya jina lake kujumuishwa kwenye orodha ya wawaniaji.

Ikionekana kuangazia chaguzi ndogo zijazo na pia uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022, tume ya EACC imesema watu wanaotuhumiwa kuhusika kwenye ufisadi hawatakubaliwa kuwania wadhifa wowote.

Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo Twalib Mbarak amesisitiza kwamba wawaniaji kwenye uchaguzi sharti watimize matakwa ya sura ya sita ya katiba ya Kenya kuhusu uongozi na maadili.

Taarifa ya tume hiyo imejiri siku mbili baada ya aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinard Waititu aliyetimuliwa kwa madai ya ufisadi kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha ugavana wa Kaunti ya Nairobi.

Nia ya Waititu ya kuwania wadhifa huo imetiliwa shaka na wengi, ikizingatiwa kuwa aliondolewa mamlakani kwa tuhuma za matumizi mabaya ya mamlaka na utovu wa maadili.

EACC imeshikilia kwamba japo jukumu la kikatiba la kuidhinisha wagombea wa nyadhifa mbali mbali kwenye uchaguzi ni la IEBC, EACC itahakikisha kwamba sura ya sita ya katiba inazingatiwa vilivyo.

Ili kuhakikisha hilo linatimia, Mbarak amefichua kwamba tume hiyo itawafanyia uhakiki wa kimaadili wagombea wote wa chaguzi zijazo kisha iwasilishe uamuzi wake kwa IEBC.

Mkuu huyo wa EACC ameeleza kwamba tume hiyo pia ina jukumu la kikatiba la kuishauri IEBC kuhusu maadili ya mtu anayenuia kugombea wadhifa wowote.

Aidha, EACC imewahimiza Wakenya kuhakikisha wanachagua viongozi wenye maadili, ikihoji kwamba kuwapa uongozi watu wenye tabia za kutiliwa shaka kutasababisha ufisadi katika usimamizi wa rasilimali za umma.

Taarifa ya tume ya EACC inaonekana kuzima ndoto ya Waititu ya kuwania kiti hicho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *