Klabu ya Simba imeandikisha historia baada ya kusajili wa ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Platinum Fc ya Zimbabwe na kufuzu hatua ya makundi ya kombe la ligi ya mabingwa Afrika katika mchuano wa marudio uliosakatwa Jumatano jioni katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar.
Difenda Erasto Nyoni aliwanyanyua mashabiki takriban 30,000 wa wekundu wa msimbazi waliofurika uwanjani kwa bao la kwanza kupitia mkwaju wa penati wa dakika ya 40 huku wakienda mapumziko kwa uongozi huo.
Kipindi cha pili Mnyama Simba alirejea kwa uchu wa mashambulizi yaliyozalisha goli la pili lililopachikwa kimiani na beki Shomari Kapombe katika dakika ya 61 naye Juma Bocco akapiga bao la tatu dakika ya 91 huku Cletus Chama akifunga karamu kwa bao la nne dakika ya 94.
Simba watakuwa wakipiga hatua ya makundi ya kombe hilo lenye donge nono kwa mara ya pili na ya kwanza tangu mwaka 2003 ikiwa pia timu ya pekee kutoka Afrika Mashariki kucheza hatua hiyo.
Simba walikuwa wamepoteza duru ya kwanza bao 1-0 ugenini hivyo basi wapiga delji hadi hatua ya makundi kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-1 dhidi ya Platinum.