Sikupata Covid – 19 Kenya, Ashanti

Ashanti, mwanamuziki wa Marekani ambaye alizuru Kenya hivi maajuzi amekana tetesi kwamba aliambukizwa Covid – 19 akiwa Jijini Nairobi. Mwanadada huyo wa miaka 40 alitumia akaunti yake ya Instagram kuelezea hali ilivyo.

Kulingana naye, alipata ugonjwa huo baada ya kukumbatia mmoja wa watu wa familia yake aliporejea nyumbani baada ya kuzuru Kenya.

Ashanti alielezea kwamba aliyemwambukiza ugonjwa huo hata yeye hakujua kwamba anao. Mwanamuziki huyo alitumia nafasi hiyo kuzungumzia madai kwamba anajisingizia kuwa na ugonjwa wa Covid 19 ili akose kuhudhuria shindano kati yake na mwanamuziki Keyshia Cole.

Shindano hilo la Verzuz linalodhaminiwa na kampuni ya Apple sasa litafanyika tarehe 9 mwezi Januari mwaka ujao wa 2021. Kabla ya kuahirisha, waandalizi walikuwa wamejaribu kila njia kuona kwamba onyesho linaendelea lakini kukatokea changamoto kadhaa.

Walihisi kwamba mashabiki wangehisi wamedanganywa ikiwa Ashanti angefanyia nyumbani na Keyshia awe studioni.

Ashanti alielezea kwamba hana maumivu yoyote lakini hana uwezo wa kunusa, kuonja chochote na ana mafua kidogo tu na kwamba wote aliosafiri nao walipimwa na kupatikana bila virusi vya Corona.

Alisisitiza kwamba Covid 19 ni ugonjwa wa ukweli kwa wanaouchukulia kuwa mzaha kwa hivyo watahadhari wasije wakaugua ugonjwa huo ambao unaua watu wengi nchini Mrekani na kwingineko ulimwenguni.

Mwanadada huyo alitaja watu wa Nairobi ambao alishukuru kwa upendo na akaahidi kurejea akishapona ugonjwa huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *