Sihitaji walinzi nalindwa na Mungu, Koffi Olomide

Mwanamuziki wa muda mrefu wa nchi ya Congo Koffi olomide au ukipenda Le Grand Mopao au Boss ya Mboka amefichua kwamba yeye huwa hatembei na walinzi kwani anaamini kwamba analindwa na Mungu.

Koffi aliyasema hayo kwenye studio ya Wasafi Fm wakati yeye na Diamond Platnumz walikuwa wanazindua kibao chao kwa jina “Waaa”.

Hapo hapo kwenye kipindi cha ‘The Switch’ ilifichuka kwamba Koffi ana ujuzi wa kiwango cha juu katika mchezo wa Karate maanake ana “Black Belt”.

Alisema kwamba akikasirika yeye huwa mbaya na anaweza kuumiza mtu na ndio maana wakati wote anajituliza na kupoesha hasira.

Ama kweli ana ujuzi huo ikikumbukwa teke aliyomrushia mmoja wa wacheza densi wake katika uwanja wa ndege nchini Kenya kitendo kilichosababisha atimuliwe hata kabla ya onyesho lake.

Boss ya Mboka anatarajiwa kuendelea kukaa nchini Tanzania kwa muda kulingana na usemi wa Diamond kwamba ana video nyingine anafaa kuandaa.

Duru za kuaminika zinaarifu kwamba video hiyo ni ya kibao cha Koffi na Nandy au ukipenda African Princess. Wakati wa mahojiano Koffi alifichua kwamba ameshirikiana pia na Nandy kwenye muziki na dada huyo amekuwa akimsukuma wafanye video lakini akampa Diamond nafasi ya kwanza.

Alipoulizwa kuhusu kitu ambacho amependa sana nchini Tanzania, Koffi alisema kwamba ni wanawake ambao kulingana naye ni warembo.

Tukio jingine ambalo linatarajiwa kumweka Koffi nchini Tanzania ni ziara inayofanywa na Wasafi Media kwa ushirikiano na Tigo na Pepsi ambapo Diamond alimwalika kwenye ziara ya mwishi mjini Daressalaam. Jana mwanamuziki huyo alikwenda kwenye mkahawa wa Shilole kwa jina Shishi food kwa chakula cha mchana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *