Categories
Habari

Shule ya Msingi ya Lporos huko Samburu yafungwa kwa hofu ya maambukizi ya Corona

Shule ya Msingi ya Lporos katika eneo la Maralal, Kunti ya Samburu imefungwa kwa muda baada ya mwalimu mmoja kuambukizwa virusi vya Corona.

Kwa sasa mwalimu huyo anapokea matibabu katika hospitali moja katika Kaunti ya Nakuru.

Kulingana na Afisa Mkuu wa Elimu katika Kaunti ya Samburu Allan Omondi, shule hiyo imefungwa ili kutoa nafasi ya kupilizwa kemikali ya kuua virusi hivyo.

Omondi amesema kuwa wanafunzi hao wa gredi ya nne na darasa la nane wanatarajiwa kurejea shuleni baada ya siku mbili, kwa ushauri wa maafisa kutoka Wizara ya Afya.

“Baada ya kupulizwa kemikali, tunatarajia kwamba wanafunzi wetu watarudi shuleni baada ya masaa 48,” ameeleza Omondi.

Aidha, walimu tisa na mfanyikazi mwengine mmoja wa shule hiyo wamefanyiwa upimaji wa virusi hivyo na wanasubiri matokeo.

Wazazi wa watoto hao wameitaka serikali kusaidia katika juhudi za kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo kwa ajili ya usalama wa wanafunzi shuleni.

“Serikali ichukue hatua ili watoto watakaporudi shuleni wazazi wajue watoto wao wako salama,” amesema mzazi mmoja ambaye pia ni mkazi wa eneo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *