Shule bora ya Msingi yapoteza sehemu ya uwanja Murang’a kufuatia mzozo wa ardhi

Wazazi na walimu wa Shule ya Msingi ya Technology katika kaunti ya Murang’a walipigwa na butwaa baada ya mkazi mmoja kutwaa sehemu ya uwanja wa shule hiyo.

Mkazi huyo aliyekuwa amejihami na agizo la mahakama aliwatuma watu kuweka ua katika sehemu ya uwanja wa shule hiyo na kuwaacha wanafunzi na mahali padogo pa kuchezea.

Kipande hicho tata cha ardhi kilikabidhiwa shule hiyo mwaka wa 1990 kwa upanuzi baada ya mwingilio wa aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Murang’a wa wakati huo.

Kipande hicho cha ardhi kilikuwa kifidiwe na ardhi mbadala na lililokuwa baraza la kaunti ya Murang’a.

Shule hiyo ya msingi ilianzishwa mwaka wa 1983 karibu na mji wa  Murang’a kwenye ardhi iliyokuwa ya Chuo cha Teknolojia cha Murang’a ambacho kilipandishwa ngazi na kuwa Chuo Kikuu cha Teknolojia cha  Murang’a.

Baada ya kuongezeka kwa wanafunzi katika shule hiyo, vipande vitatu vya ardhi vilivyo karibu na shule hiyo vilitwaliwa ili kupanua uwanja wa shule hiyo.

Vipande viwili vya ardhi vilikuwa vya shirika la Kenya Industrial Estates KIE huku kingine kikisemekana kuwa cha mkazi kwa jina Julius Ngige Munjunga.

Ardhi mbadala ilitarajiwa kutolewa kufidia Shirika la KIE na Munjunga na lililokuwa baraza la kaunti ya Murang’a.

Shirika la KIE lilipata ardhi mbadala na lakini Munjunga anadai kuwa hajawahi kufidiwa.

Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo Harrison Mwangi ameeleza kuwa shule hiyo imekuwa ikishindana na Munjunga mahakamani tangu mwaka wa 2013 kuhusu mzozo huo hadi mwaka wa 2017 ambapo Munjunga alishinda kesi hiyo.

“Munjunga alijitokeza mwaka wa 2013 akidai fidia kwa ardhi aliyotoa kwa shule, jambo ambalo lilipelekea kuwasilishwa kwa kesi mahakamani. Alishinda kesi hiyo kabla shule kukata rufaa, lakini mwaka wa 2019, Mahakama ya Ardhi na Mazingira ya Kirinyaga ikahitimisha kesi hiyo kwa faida ya Munjunga,” akaeleza Mwangi.

Mwangi sasa anaomba msaada kutoka kwa serikali na wahisani akihoji kuwa shule hiyo inahitaji ardhi zaidi kwa ajili ya upanuzi wa miundo msingi, huku idadi ya wanafunzi ikiendelea kuongezeka kutokana na shule hiyo kuandikisha matokeo mazuri kwenye mitihani ya kitaifa.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *