Shughuli za upigaji kura zaendelea kwenye chaguzi ndogo tano nchini

Maelfu ya wapiga kura wanaendelea kujitokeza ili kushiriki kwenye shughuli za chaguzi ndogo katika maeneo matano mbali mbali humu nchini.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inasimamia uchaguzi mdogo wa Eneo Bunge la Msambweni katika Kaunti ya Kilifi.

Aidha, kuna chaguzi ndogo nne za Wadi za Dabaso katika Kaunti ya Kilifi, Kisumu Kaskazini katika Kaunti ya Kisumu, Kahawa Wendani iliyoko Kaunti ya Kiambu na Wundanyi/Mbale huko Taita Taveta.

Chaguzi hizo zinafanyika kwa kuzingatia kikamilifu maagizo ya Wizara ya Afya ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa COVID-19, ikiwa ni pamoja na kupimwa joto na kunawa mikono ama kutumia vieyuzi.

Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa saa kumi na mbili alfajiri na shughuli ya upigaji kura inaendelea hadi saa kumi na mbili jioni.

Wapiga kura wanatambuliwa kwa kutumia vifaa vya kielektroniki kabla kuruhusiwa kupiga kura.

Tume ya IEBC imeweka makarani maalum wa kuhakikisha kwamba watu wanavaa barakoa, wanadumisha umbali ufaao na wananawa mikono kabla kuruhusiwa kuingia katika sehemu za kupiga kura.

Hata hivyo, macho yote yameelekezwa kwenye uchaguzi wa Msambweni ambako wakazi wanamchagua mbunge mpya kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa eneo hilo Suleiman Dori.

Ushindani mkali katika uchaguzi huo ni kati ya Omari Boga wa chama cha ODM na mwaniaji huru Feisal Bader anayeungwa mkono na Naibu Rais William Ruto.

Usalama umeimarishwa katika eneo hilo ili kuhakikisha kwamba zoezi hilo linafanyika katika utaratibu ufaao na bila fujo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *