Shughuli ya ukusanyaji saini za BBI yazinduliwa rasmi Mombasa

Wakazi wa Kaunti ya Mombasa wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye shughuli ya ukusanyaji saini za mpango wa BBI.

Kwenye hafla ya uzinduzi wa shughuli ya ukusanyaji saini katika kaunti hiyo, viongozi wa eneo hilo wamepongeza mapendekezo kwenye ripoti ya BBI iliyorekebishwa.

Hafla hiyo iliyofanyika Jumamosi ilihudhuriwa na Seneta wa Mombasa Mohamed Faki, Mbunge wa Likoni Mishi, Mbunge wa Jomvu Badi Twalib, Mwakilishi wa Wanawake Aisha Mohammed na Wawakilishi kadhaa wa Wodi wakiongozwa na Naibu Spika katika Bunge la Kaunti ya Kilifi, Fadhili Makarani.

Viongozi hao wamekariri kuwa marekebisho ya katiba yatatatua dhuluma za jadi ambazo zimekuwa zikiwakumba wakazi wa Pwani kwa miaka mingi pamoja na maswala mengine nyeti kama vile shughuli za Uchumi wa Baharini, uchoraji wa mipaka ya ardhi na swala la ukosefu wa ajira.

“Wakazi wa Pwani watafaidika sana kutokana na mapendekezo ya marekebisho ya katiba kwa hivyo wanastahili kuunga mkono kikamilifu mchakato wa BBI,” akasema Seneta Faki.

Aidha, Faki ametoa wito kwa serikali ya kitaifa kuhamisha usimamizi wa huduma za Ferry hadi kwa serikali ya Kaunti ya Mombasa.

Kwa upande wake Mbunge wa Likoni Mishi Mboko amesisitiza kwamba BBI inalenga kuimarisha zaidi katiba iliyopo sasa na akawahimiza Wakenya wote kuunga mkono mpango huo.

Amesema kuwa marekebisho yaliyopendekezwa yatasaidia kuleta usawa katika ugavi wa rasilimali na ujumuishaji unaolenga kumaliza chuki na machafuko baina ya jamii mbali mbali kila baada ya uchaguzi mkuu humu nchini.

Mboko ameongeza kuwa wanawake kote nchini pia watapata manufaa mengi kutokana na mchakato huo unaonuia kutatua changamoto ya usawa wa kijinsia na uwakilishi duni.

Mshirikishi wa Usalama katika eneo la Pwani John Elungata amewahakikishia wakazi kuwa marekebisho yaliyopendekezwa ya katiba yataleta nafuu katika kaunti hiyo kutokana na dhuluma za jadi za uchaguzi ili kukuza mazingira ya amani na uwiano.

Elungata amehimiza wakazi wa eneo zima la Pwani kushiriki kikamilifu kwenye zoezi la ukusanyaji saini, akihoji kuwa tayari kaunti zote sita za Pwani zimepokea fomu za kutosha kwa ajili ya zoezi hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *