Shindano la muziki la “Old Mutual amazing Voices”

Awamu ya pili ya shindano la ‘Old Mutual Amazing Voices’ imeanza na kwa sasa makundi ya muziki yanahitajika kuwasilisha video zao kwa uteuzi kwenye jukwaa lililoko kwenye tovuti ya shindano.

Mwaka huu mambo ni tofauti kidogo kutokana na janga la virusi vya Corona ulimwenguni kote. Mwaka jana makundi yalijitokeza mbele ya majaji ambapo waliteua makundi 12 kuingia kwa shindano hilo.

Shindano hilo huwa la vipindi kumi na vitatu vya runinga na linahusu makundi ambayo hayajakiandikisha na kampuni yoyote ya kusimamia wanamuziki kutoka nchi za Afrika.

Ghana, Kenya, Zimbabwe na Afrika Kusini zilimenyana mwaka jana ambapo kundi la Kenya kwa jina ‘Wanavokali’ liliibuka mshindi na kutia kibindoni dola laki moja za kimarekani ambazo ni sawa na shilingi milioni kumi za Kenya.

Waimbaji kwenye kundi hilo ni Ythera, Riki Msanii, Chepkorir, Lena Gayah, Rui na Mellah.

Mwaka huu nchi ya Ghana imeongezeka kwenye orodha ya zile ambazo ziko mbioni kushinda dola hizo laki moja.

Makundi yanahitajika kuingia kwenye ukaguzi wa uteuzi kupitia kutuma video zinazoonyesha uwezo wao kwa kuimba na kutumbuiza. Zoezi la ukaguzi lilianza tarehe ishirini na nane mwezi Oktoba mwaka huu na litaendelea hadi tarehe 26 mwezi Novemba mwaka huu wa 2020.

Shindano linahusu aina tatu za muziki ambazo ni muziki wa injili, muziki wa pop na mtindo wa R&B.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *