Shebesh ataka viongozi wa kitamaduni waingilie kati ili kukabiliana na ukeketaji

Katibu Mkuu Mwandamizi katika Wizara ya Vijana na Jinsia Rachel Shebesh amesisitiza umuhimu wa viongozi wa kitamaduni kuwa katika msitari wa mbele kwenye vita dhidi ya ukeketaji.

Akizungumza Mjini Narok baada ya kukutana na viongozi wa kitamaduni wa jamii ya Maasai, Shebesh amekiri kwamba mikakati ya kuwahusisha wazee italeta mafanikio katika kampeni ya kuangamiza ukeketaji humu nchini.

“Tumekuwa tukishirikisha afisi za Kamishna wa Kaunti, wanawake na makanisa lakini hatujawashirikisha viongozi wa kitamaduni ambao ni nguzo muhimu sana katika kukabiliana na tamaduni hiyo potofu,” amesema Shebesh.

Shebesh ameeleza kuwa vita dhidi ya ukeketaji havilengi kuwakamata wahusika bali kuhamasisha jamii ili zikubaki kwa hiari kuacha ukeketaji ambao umelaumiwa kwa kusababisha wasichana wengi kuacha shule.

Katibu huyo alikuwa ameandamana na Mwenyekiti wa Bodi ya Kukabiliana na Ukeketaji Agnes Pareiyo pamoja na Afisa Mkuu Mtendaji Benedict Loloju, miongoni mwa viongozi wengine.

Pareiyo amekiri kwamba kuna changamoto kubwa katika vita dhidi ya ukeketaji lakini hatua ya kuwahusisha viongozi wa kitamaduni itasaidia sana kuangamiza tamaduni hiyo miongoni mwa jamii mbali mbali.

Kwenye kongamano la ‘Women Deliver’ lililoandaliwa nchini Canada mwaka wa 2019, Rais Uhuru Kenyatta aliapa kuangamiza ukeketaji humu nchini kufikia mwaka wa 2022.

Ukeketaji umeorodheshwa miongoni mwa sababu kuu zinazopelekea mimba na ndoa za mapema kwa wasichana wadogo kwani wasichana hao huchukuliwa kuwa tayari kuolewa baada ya kufanyiwa ukeketaji.

Ripoti za tafiti mbali mbali pia zimefichua kwamba vifo vya watoto wachanga wakati wa kuzaliwa kwao ni vingi katika maeneo ambayo yanajulikana kwa kuendeleza ukeketaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *