Serikali yatakiwa kuimarisha hali ya makazi ya Polisi

Kamati ya Bunge kuhusu Utawala na Usalama wa Kitaifa imeshauri serikali kubadili sera zake kuhusu makazi ya maafisa wa polisi.

Hii imetokana na kwamba maafisa wengine wa polisi wanalazimika kuishi nje ya vituo vyao kutokana na ukosefu wa makazi ya kutosha katika vituo hivyo.

Kulingana na Mwenyekiti wa kamati hiyo aliye pia Mbunge wa Kiambaa Paul Koinange, mpangilio huo ni tisho kwa usalama wa maafisa hao hasa kutoka kwa makundi ya wahalifu.

Kwa mara nyengine, mwenyekiti huyo amelalamikia hali duni ya vituo vya polisi nchini, akitoa mfano wa Kituo cha Wanguru.

Koinange amesema kuwa hali ya mazingira ya kituo hicho ni hatari kwa maafisa wa polisi pamoja na washukiwa wanaozuiliwa kwenye kituo hicho huku akimtaka Waziri wa Usalama wa kitaifa Dkt. Fred Matiangi kurekebisha hali hiyo.

Kauli yake imeungwa mkono na Mbunge wa Mwea Kabinga Wachira, aliyeitaja hali ya kituo hicho kuwa ya kusikitisha na isiyofaa kwa binadamu.

Amesema majengo ya kituo hicho na pia vituo vyengine kote nchini ni yale yaliyojengwa wakati wa ukoloni na yanahitaji kufanyiwa ukarabati wa haraka.

Wachira amesisitiza kwamba maafisa wa polisi wanafaa kupewa makazi katika vituo vyao ili kurahisisha uwezo wao wa kushughulikia dharura wakati wowote.

Kamati hiyo imekuwa ikikagua vituo vya polisi nchini na kupendekeza fedha zaidi kutengwa ili kuimarisha hali ya vituo hivyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *