Serikali yaonya dhidi ya uchochezi katika mikutano ya umma

Baraza la Kitaifa la Ushauri kuhusu maswala ya Usalama limetoa onyo kali kwa viongozi wanaowachochea Wakenya wakati wa mikutano ya hadhara.

Akiongea na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa baraza hilo Joseph Kinyua, ambaye pia ni Mkuu wa Utumishi wa Umma, ameagiza kwamba mikutano yote ya hadhara iandaliwe kuambatana na sheria kuhusu usalama wa umma, akionya kuwa wakiukaji wa agizo hilo wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

Kinyua ameagiza kuwa mtu yeyote anayenuia kuandaa mkutano sharti atoe taarifa kwa idara ya usalama angalau siku tatu kabla mkutano huo.

“…atoe taarifa kwa OCS kuhusu nia hiyo katika muda wa angalau siku tatu lakini usiozidi siku 14 kabla siku ya mkutano wa hadhara,” amesema.

Amesema taharuki ya kisiasa inayoshuhudiwa humu nchini inaibua migawanyiko kati ya mirengo pinzani ya kisiasa, hali aliyoitaja kuwa tishio kwa usalama wa nchi.

Kinyua amesema kila kiongozi atawajibikia matamshi yake binafsi, huku akitoa wito kwa Wakenya kumripoti kwa maafisa wa usalama yeyote anayetoa matamshi ya chuki na uchochezi.

Hata hivyo, ametoa wito wa kuheshimiwa kwa uhuru wa kujieleza kwa kila mmoja.

Pia amevitahadharisha vyombo vya habari vinavyotangaza au kuchapisha taarifa  za uchochezi ama matamshi ya chuki.

Wakati uo huo, Kinyua amewataka wanaotumia mitandao ya kijamii kuwajibikia taarifa watakazochapisha huku wasimamizi wa mitandao hiyo wakitakiwa kudhibiti mijadala inayoendelezwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *