Serikali yaimarisha uvuvi kwenye vina virefu baharini

Waziri wa kilimo, ufugaji na shughuli za uvuvi Peter Munya amezindua mashua tatu za kisasa ambazo zitawezesha wavuvi katika eneo la pwani kuvua samaki kwenye vina virefu baharini.

Munya amesema mashua hizo tatu zitagawiwa wavuvi katika kaunti za Mombasa, Kilifi na Lamu kuwawezesha kuvua samaki kwenye vina virefu.

Munya alidokeza kuwa mashua nyingine mbili za kisasa zitanunuliwa na kugawiwa wavuvi wa Lamu na Tana River.

Munya alizindua mashua hizo katika eneo la Liwatoni bandarini Mombasa ambapo alisema shughuli za uvuvi zitaimarika humu nchini na kupiga jeki ustawi wa kiuchumi na kijami.

Waziri huyo alisema uzinduzi huo unajiri wakati ambapo wavuvi 186 wa eneo hilo wamepokea mafunzo ya uvuvi katika vina virefu katika chuo cha maswala ya baharini cha Mombasa.

Munya alisema kuwa wavuvi katika eneo hilo wamekuwa wakikabiliwa na ukosefu wa mashua za kuwawezesha kuvua samaki kwenye vina virefu baharini, shughuli ambayo imeachiwa wavuvi wa kigeni walio na mashua bora.

Waziri huyo alidokeza kuwa serikali imejitolea kuwekeza zaidi katika sekta ya uvuvi ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika pato la jumla la taifa sawia na kuongeza nafasi za ajira.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *