Categories
Habari

Serikali yabuni kamati yakushughulikia Usalama na Utangamano wa umma

Baraza la mawaziri limeidhinisha maagizo yaliotolewa na kamati ya kitaifa ya ushauri wa maswala ya usalama, kuhusu uzingatiaji wa sheria ya usalama wa umma wakati wa mikutano ya hadhara na maandamano.

Mkutano huo  wa kila wiki ulioongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, uliidhinisha kubuniwa mara moja kwa kamati inayojumuisha vitengo mbali mbali.

Jukumu la kamati hiyo likiwa kuhakikisha kuwa usalama na untangamano wa nchi hii havitishiwi.

Vile vile kamati hiyo itakuwa na jukumu la kuchunguza,kunakili na kuhakikisha uzingatifu wa sheria kuhusu usalama wa umma katika mikutano ya hadhara na vyombo vya habari,ikiwemo mitandao ya kijamii.

Mkutano huo wa baraza la mawaziri umeandaliwa wakati ambapo nchi hii inaghubikiwa na taharuki ya kisiasa.

Kamati hiyo itakuwa na wawakilishi kutoka idara mbali mbali za serikali kama vile wizara ya usalama wa kitaifa, ile ya habari na mawasiliano pamoja na tume ya utangamano na maridhiano ya kitaifa.

Wakati wa mkutano huo, baraza la mawaziri lilidokeza taharuhi za kisiasa zinazoongezeka humu nchini na ambazo zimetishia usalama, amani na umoja wa taifa hili katika muda wa mwezi mmoja uliopita.

Siku ya Jumatano baraza la kitaifa la ushauri kuhusu maswala ya usalama lilitoa onyo kali kwa viongozi wanaowachochea vijana wakati wa mikutano ya hadhara.

Mwenyekiti wa baraza hilo Joseph Kinyua ,ambaye pia ni mkuu wa utumishi wa umma,aliagiza kwamba mikutano yote ya hadhara iandaliwe kuambatana na sheria kuhusu usalama wa umma.

Alisema taharuki ya kisiasa inayoshuhudiwa hapa nchini inaibua migawanyiko kati ya mirengo pinzani ya kisiasa,hali alitaja kuwa tishio kwa usalama wa nchi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *