Categories
Habari

Serikali ya Kaunti ya Kilifi yazindua mpango wa chanjo kwa mifugo

Serikali ya kaunti ya Kilifi imeanzisha mpango wa kuwapa chanjo zaidi ya mifugo laki tano ili kuzuia vifo vinavyotokana na magonjwa mbali mbali yanayowaathiri mifugo.

Mpango huo wa utoaji chanjo utatekelezwa kwa mwezi mmoja kabla ya kuanza kwa mvua kubwa ili kuzuia vifo vya mifugo katika maeneo yote ya kaunti hiyo.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa shughuli hiyo huko  Tsangatsini katika Kaunti Ndogo ya Kaloleni, Afisa Mkuu kuhusu ustawi wa mifugo Fredrick Kaingu amesema kuwa kaunti hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ya kudhibiti magonjwa yanayoathiri mifugo.

“Tunalenga Kaunti nzima ya Kilifi katika Kaunti ndogo zote saba ambapo tutatoa chanjo zitakazolenga takribani asilimia 50 ya mifugo wote,” amesema Kaingu.

Amesema kuwa kichinjio cha  Malindi na maduka yote ya uuzaji nyama katika kaunti hiyo ndogo yalifungwa mwaka uliopita kufuatia chamko la ugonjwa wa homa ya Rift Valley hali ambayo amesema inaweza kuzuiwa kupitia utoaji chanjo.

Kaingu amesema mipango inatekelezwa kuanzisha maeneo ambako magonjwa yamedhibitiwa kikamilifu katika kaunti hiyo ili kuzuia kuenea kwa magonjwa ya mifugo.

Serikali hiyo inapanga kutumia shilingi milioni 60 kuhamishwa na kujenga vichinjio vipya katika maeneo ya Malindi na Mariakani.

Afisa mmoja wa matibabu ya mifugo katika kaunti ya Kilifi, Dkt. Carolyne Asanyo amesema kuwa wakulima wamekuwa wakipata hasara kufuatia kufungwa kwa masoko makuu akisema kuwa hatua za kudhibiti magonjwa hayo zilizochukuliwa na serikali ya kaunti hiyo zitawakinga wakulima dhidi ya vifo vya mifugo wao katika msimu huu ambapo wanatarajia chamko la magonjwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *