Serikali ya Kaunti ya Garissa yazindua mpango wa miaka mitano ya lishe bora kwa wakazi

Serikali ya Kaunti ya Garissa imezindua mpango wa miaka mitano wa kushughulikia tatizo la ukosefu wa lishe bora katika kaunti hiyo.

Akizungumuza kwenye hafla ya uzinduzi wa mpango huo katika hoteli moja mjini Garissa, Waziri wa Afya wa kaunti hiyo, Roble Nunow, alisema kuwa ukosefu wa lishe ni changamoto ya afya ya umma.

Aidha, Roble alisema changamoto ya utapia mlo inarudisha nyuma ufanisi wa kielimu na uzalishaji wa kiuchumi na unaipa serikali na pia familia nyingi gharama za kimatibabu.

“Tatizo la utapia mlo sio tu changamoto katika uafikiaji wa ruwaza ya mwaka wa 2030, bali pia ni kikwazo kwenye harakati zetu za kuafikia malengo ya maendeleo endelevu,” akasema waziri huyo.

Alisema mpango huo utaboresha maisha ya wakazi kwa minajili ya kuafikia mabadiliko ya kiuchumi.

Roble alisema mpango huo wa kati ya mwaka wa 2019 hadi 2023 unaambatana na ule wa serikali ya kitaifa wa kushirikisha maswala ya lishe katika mipango ya maendeleo ya magatuzi.

Kulingana na uchunguzi wa hali ya afya ya wakazi wa kaunti hiyo wa mwaka wa 2014, yamkini wakazi asilimia 15.6 walipatikana na hali ya kutoweza kukua vyema kutokana na ukosefu wa lishe bora.

Uchunguzi mwingine uliofanywa mwaka wa 2019 ulibaini kuwa asilimia 17.2 ya watoto wa chini ya umri wa miaka mitano walikuwa na tatizo la ukosefu wa lishe.

Afisa Mkuu wa Afya wa kaunti hiyo Hassan Anshur aliahidi kuwa wataimarisha utoaji wa huduma za lishe na pia matumizi ya huduma hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *