Serikali kushirikiana na Kanisa katika utoaji huduma kwa Wakenya

Rais Uhuru Kenyatta amewahakikishia Wakenya kwamba serikali yake itaendelea kushirikiana na kanisa katika kuwahudumia Wakenya.

Rais amesema kwa miaka mingi kanisa limekuwa likishirikiana na serikali katika utekelezaji wa mipango mbali mbali ya kuinua hali ya maisha ya Wakenya, ushirikiano ambao amesema unafaa kuimarishwa zaidi.

“Sio injili pekeake inayoenezwa na kanisa. Kanisa limechanganya uenezaji injili, elimu na afya. Limetibu roho, akili na mwili,” amesema Rais Kenyatta.

Amesema hayo katika kanisa la PCEA la Tumutumu katika Kaunti ya Nyeri, ambako amehudhuria ibada maalumu ya kuadhimisha miaka 100 tangu kutawazwa kwa kundi la kwanza la wazee 43 kanisa.

Rais amelipongeza kanisa hilo kwa mchango wake mkubwa katika ustawishaji sekta za elimu na afya humu nchini.

Amesema ni kupitia uwekezaji wa kanisa katika taasisi za elimu ambapo waasisi wa nchi hii, miongoni mwao Mzee Jomo Kenyatta walipata fursa ya kuenda shule.

Wakati wa ziara hiyo rais ameahidi mchango wa shillingi milioni 100 kwa kanisa hilo ili kukamilisha kazi inayoendelea ya upanuzi wa Hospitali ya Misheni ya PCEA, Tumutumu.

Kadhalika rais ametangaza kwamba serikali ina mipango ya hati kwa Chuo Kikuu cha PCEA kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *