Serikali kusambaza shilingi bilioni 19 kwa shule za umma ili kufadhili mpango wa elimu bila malipo

Huku tarehe ya ufunguzi wa shule ikikaribia, serikali iko mbioni ili kusambaza shilingi bilioni 19 kwa shule za umma chini ya mpango wa elimu ya msingi bila malipo.

Waziri wa Elimu Profesa George Magoha amefichua kwamba mashauriano yanaendelea kati ya Wizara ya Elimu na ile ya Fedha kuhakikisha kwamba fedha hizo zinasambazwa kwa wakati ufaao ili kuwezesha shule kufanyaa maandalizi ya ufunguzi.

Shule kote nchini zinatarajiwa kufunguliwa Jumatatu tarehe nne mwezi Januari baada ya kufungwa kwa muda mrefu kufuatia janga la COVID-19.

Kulingana na Magoha, shilingi bilioni nne zitaenda kwa shule za msingi huku shilingi bilioni 15 zikipelekwa kwenye shule za upili.

Magoha amewataka wakuu wa shule kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa njia ifaayo, akionya kwamba wale watakaopatikana wamefuja fedha hizo watachukuliwa hatua kali.

Ametoa hakikisho kwamba serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha kwamba shule ziko tayari kwa ufunguzi, huku akiwarai wazazi wawatayarishe watoto wao ili wafike shuleni siku hiyo.

Akizunguma katika Shule ya Msingi ya Obola, iliyoko katika Kaunti Ndogo ya Seme, Kaunti ya Kisumu, Magoha amesema kwamba wizara yake inashauriana na ile ya usalama ili kuhakikisha kwamba wanafunzi wote wanarejea shuleni tarehe nne Januari.

Amekiri kwamba janga la COVID-19 limeathiri uchumi wa wazazi kwa hivyo akawaomba wakuu washule wasiwarudishe nyumbani watoto kwa sababu ya karo bali washauriane na wazazi kuhusu njia za ulipaji wa karo hizo.

Ameongeza kuwa wanafunzi waliokuwa wakisomea shule za kibinafsi ambazo kwa sasa zilifilisika watasajiliwa katika shule za umma na kwamba watahiniwa wa shule kama hizo wataruhusiwa kufanya mitihani ya kitaifa katika shule za umma.

Magoha vile vile amewataka wazazi wawape watoto wao barakoa ili wajikinge kutokana na maambukizi ya COVID-19.

Amesema serikali itatoa msaada wa barakoa kwa wanafunzi milioni tatu wenye mahitaji.

“Tayari tuko na barakoa milioni mbili kwa ajili ya wanafunzi maskini na bado tunashauriana na Kampuni ya Rivatex ili zile milioni moja zilizobaki zipatikane kabla shule kufunguliwa,” akasema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *