Serikali kupanda miti katika maeneo yenye vyanzo vya maji
Wizara ya mazingira na misitu imeanzisha mpango kabambe wa upanzi wa miche katika maeneo yenye vyanzo vya maji.
Waziri mwandamizi katika wizara hiyo Dkt.Chris Kiptoo alishuhudia kutiwa saini kwa mkataba wa makubaliano kuhusu jambo hilo kati ya Huduma ya Misitu nchini-KFS na shirika la kitaifa la uhifadhi wa vyanzo vya maji-KTWA,huku akisema ustawishaji wa misitu ni muhimu kwa uhifadhi wa mazingira.
Pande zote mbili zilikubaliana kutumia kipande cha ardhi cha ekari 250 kwenye msitu wa Kaptagat kwa mpango wa majaribio wa kilimo cha mianzi.
Mbegu kutokana na shamba hilo zitagawiwa wakulima katika maeneo chepechepe huko Nandi,Uasin Gishu,Trans Nzoia na Elgeyo Marakwet ambako hutokea maporomoko ya udongo ya mara kwa mara.
Akiongea katika shule ya msingi ya Kaptagat Dkt.Kiptoo alitangaza mpango mkuu wa kurejesha na kuustawisha tena msitu wa Cherengany na eneo la milima ya Elgeyo ambalo litatangazwa hivi karibuni kuwa chanzo muhimu cha maji kwa mujibu wa arifa iliochapishwa kwenye gazeti rasmi la Serikali.
Wakatu huo huo wakazi wa kaunti ndogo ya Buuri,kaunti ya Meru wamehimizwa kuhifadhi mazingira kwa kuzingatia upanzi wa miche.
Akiongea alipokuwa akigawa miche kwa wakulima,mwakilishi maalum wa wadi, Joy Karambu aliwataka wakazi wa sehemu hiyo kupanda miche zaidi ili kuongeza eneo la msitu katika sehemu hiyo.
Karambu alisema sehemu kubwa ya kaunti hiyo ndogo haina msitu,jambo ambalo limesababisha mmomonyoko wa udongo.
Alisema hali hiyo isipozuiliwa itasababisha ukame na uhaba wa chakula katika kaunti hiyo.
Aliongeza kusema kuwa miti ni muhimu kwa kuwa husaidia kuvutia mvua.
Karambu aliwataka wakulima katika sehemu hyo pia kupanda miche kwenye sehemu za mashamba yao ili kuafikia kiwango cha aslimia 10 ya eneo la msitu humu nchini.
Aliwaonya wale wanaoishi kwenye misitu ya serikali na wale wanaokata miti kiholela kwenye ardhi ya umma kwamba watachukuliwa hatua za kisheria na ardhi hiyo kutwaliwa na serikali.