Categories
Habari

Safari ya kumsaka Jaji Mkuu mpya yang’oa nanga

Idara ya Mahakama imeaanzisha mchakato wa kumtafuta mrithi wa David Maraga kwenye cheo cha Jaji Mkuu humu nchini.

Kaimu Jaji Mkuu Philomena Mwilu amechapisha arifa ya kutangaza nafasi hiyo kwenye gazeti rasmi la serikali na kutoa fursa kwa wale wanaotaka kuwania wadhifa huo kutuma maombi.

Wale watakaopeleka maombi ya kuwania wadhifa huo wataorodheshwa kwa mahojiano na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC).

Baada ya kukamilisha mahojiano, tume hiyo inatarajiwa kuwasilisha bungeni, jina la mtahiniwa atakayefanikiwa ili kusailiwa na kuidhinishwa kabla ya kuteuliwa rasmi na RaisUhuru Kenyatta.

Masharti ya kuteuliwa katika wadhifa wa jaji mkuu ni pamoja na ujuzi wa angalau miaka 15 kama jaji wa mahakama inayotambulika au msomi mwenye hadhi kuu, afisa wa maswala ya kisheria, mhudumu wa kisheria ama ujuzi mwingineo katika nyanja husika za kisheria.

Hatua hiyo inafuatia kustaafu kwa aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga mnamo tarehe 11 Januari mwaka huu, baada ya kutimiza miaka 70.

Kulingana na kifungu cha 167 cha katiba, sehemu ya pili, jaji mkuu atahudumu kwa kipindi kisichozidi miaka kumi au hadi kustaafu kwake atakapofikisha umri wa miaka 70 au atakapochagua mwenyewe kustaafu mapema akiwa na umri wa miaka 65.

Maraga alikuwa jaji mkuu wa 14 hapa nchini, lakini wa tatu chini ya katiba mpya ya mwaka wa 2010 baada ya kumrithi Willy Mutunga mnamo mwaka wa 2016.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *