Sabina Chege atishia kuongoza maandamano dhidi ya usimamizi wa jiji la Nairobi

Mwakilishi mwanamke wa kaunti ya Murang’a Sabina Chege anatishia kuongoza maandamano dhidi ya viongozi wa halmashauri ya usimamizi wa jiji la Nairobi.

Kulingana na Chege maandamano hayo yataandaliwa iwapo hakuna maelezo ya kuridhisha yatakayotolewa kuhusu ni kwa nini mwanamke mmoja alijifungua nje ya hospitali ya Pumwani ilhali hospitali hiyo ilifaa kutumika kwa jukumu hilo.

Mnamo siku ya Ijumaa kanda za video za mwanamke mja mzito akilia kwa maumivu alipokuwa akitafuta usaidizi wa kujifungua nje ya hospitali ya kujifungulia kina mama ya Pumwani, zilienezwa kwenye mitandao ya kijamii na kuzua malalamishi miongoni mwa wakenya.

Mwanamke huyo alijifungua kwenye kijia bila usaidizi wa kitaalamu.

Chege ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya bunge la taifa kuhusu afya sasa anatishia kuandaa maandamano dhidi ya mkurugenzi mkuu wa halmashauri ya usimamizi wa eneo la jiji la Nairobi  Abdalla Badi iwapo hakuna maelezo ya kuridhisha kutoka kwake kuhusiana na anayefaa kulaumiwa kutokana na kisa hicho cha kusikitisha.

Wakati huo huo halmashauri hiyo kwenye taarifa Jumamosi  alasiri ilisema kuwa imesikitishwa na kisa hicho.

Taarifa hiyo iliyotiwa saini na mkurugenzi wa huduma za afya, Dr. Josephine Kibaru Mbae, ilisema kuwa imethibitisha kwamba kisa hicho kilitokea siku ya Jumapili tarehe 13 mwezi huu siku mbili baada ya wauguzi kuanza mgomo baridi ambao ulikuwa umetolewa ilani ya kisheria.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *