Ruto: Sitishwi na njama za mahasimu wangu

Naibu wa Rais Dkt. William Ruto sasa anasema anafahamu kuna njama ya kumzuia kuwa Rais wa taifa hili.

Ruto alidokeza kuwa mahasimu wake wa kisiasa wanafanya kila wawezalo kuhakikisha azma yake ya kuongoza taifa hili, halifui dafu.

Naibu huyo wa Rais aliyeyasema hayo akiwa katika kaunti ya Nandi hata hivyo alisema hatishwi dhidi ya njama zozote dhidi yake.

Wanapanga njama dhidi yangu Jijini Nairobi, lakini mimi nina watu mashinani. Hakuna tatizo lolote,”alisema naibu wa rais.

Katika kile kinachoonekana kana kwamba alikashifu mkutano uliowaleta pamoja Rais Uhuru Kenyatta,Kiongozi wa ODM Raila Odinga, Kalonzo Musyoka wa Wiper, Musalia Mudavadi wa ANC, Charity Ngilu wa NARC na Moses Wetangula wa FORD-Kenya, naibu huyo wa rais alishikilia kwamba uongozi wa taifa hili sio wa kupangiwa katika mikutano ya afisini.

Wanasema watapanga serikali ijayo kutoka Jijini Nairobi, lakini nawaeleza kwamba serikali ya mwaka 2022 haiwezi kupangwa baina ya viongozi wa kikabila,” alifoka naibu wa rais.

Ruto alisema “Serikali ijayo itabuniwa na wakenya wote. Itakuwa serikali inayoelewa maswala yanayowaathiri ‘ma-hustler’.

Naibu wa rais alisema hana nia ya ugawanaji wa mamlaka ya kisiasa, akisisitiza kuwa ataendelea kuhubiri ujumbe wake wa ‘hustler’ kote nchini.

Wanauliza nitaeneza vipi ajenda yangu. Jibu langu kwao ni kwamba nilimsaidia Raila Odinga kuwa waziri mkuu na nikamsaidia Uhuru Kenyatta kuwa rais wa taifa hili. Ninajua ninachofanya,” alisema Ruto.

Kuhusu swala la BBI,naibu wa rais William Ruto alisema wakenya hawapaswi kulazimishwa kuunga mkono marekebisho ya katiba nchini. Naibu wa rais ambaye alikuwa akiongea huko Kapsabet katika kaunti ya Nandi, aliwatahadharisha baadhi ya viongozi dhidi ya kuwalazimisha wananchi kuegemea upande fulani katika mchakato wa kurekebisha katiba.

Dkt. Ruto aliwapuuzilia mbali wale wanaojaribu kumsukuma kuongoza kampeini za kupinga mchakato huo wa kurekebisha katiba huku akisema kuwa Kenya ni taifa linalozingatia maongozi ya kidemokrasia na maoni ya kila mmoja ni muhimu.

Alisema kuwa wakenya wanapaswa kuachwa kufanya maamuzi yafaayo kuhusu maswala yanayoathiri maisha yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *