Ruto na wafuasi wake wataka kura ya maamuzi ya BBI ifanyike 2022

Naibu Rais William Ruto na viongozi wengine wanaomuunga mkono wametangaza rasmi mapendekezo yao kwenye mchakato wa marekebisho ya katiba kupitia mpango wa maridhiano humu nchini, BBI.

Wakitoa taarifa hiyo katika Bustani ya Karen, viongozi hao wamependekeza kwamba kura ya maamuzi kuhusu BBI ifanyike mwaka wa 2022 pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka huo.

Viongozi hao wametetea pendekezo hilo kwa kusema kuwa litasaidia nchi hii kutumia rasilimali chache kuafikia azma ya marekebisho ya katiba.

Wamesema haina haja nchi hii kutumia shilingi bilioni 14 kwa kura ya maamuzi, mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu ambao unakadiriwa kugharimu shilingi bilioni 42 zengine, wakati ambapo nchi hii inahitaji kuelekeza rasilimali zaidi katika vita dhidi ya janga la Korona.

Viongozi hao wameandaa kikao na waandishi wa habari baada ya mkutano wao wa faragha wa kukubaliana kuhusu msimao wao kwenye swala la BBI.

Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi kutoka pembe tofauti tofauti za nchi hii wakiwemo takriban magavana wanane, manaibu gavana wanne na wabunge 146.

Viongozi hao wamesisitiza kwamba ipo haja ya kufanyia marekebisho zaidi ripoti ya BBI kuhusu yaliyomo kwenye ripoti hiyo, mfumo wa mchakato wa marekebisho ya katiba na wakati wa kufanya hivyo.

Licha ya kamati ya kitaifa kuhusu mchakato wa BBI kushikilia kwamba hakuna nafasi tena ya kuifanyia marekebisho ripoti hiyo, Naibu Rais William Ruto amesema kwamba hakuna kuchelewa katika kutekeleza jambo lililo sahihi.

“Tulipokuwa Bomas, tuliambiwa mlango umefungwa. Lakini msimamo wetu ni kwamba hatujachelewa kufanya jambo lililo sahihi,” amesema Ruto.

Aidha, Naibu Rais ametaka mfumo wa kura ya maamuzi kuhusu BBI ubadilishwe ili Wakenya wasilazimike kupiga ‘Ndio’ au ‘La’ kwenye ripoti nzima bali wawe na uhuru wa kuchagua vipengee wanavyoviunga mkono kati ya vile vilivyopendekezwa kwenye ripoti hiyo.

“Tuwe na maswali matano, sita ama saba ili tusiende katika kukataa ilhali uko na mambo ambayo ungependa yapite, ama kukubali ilhali uko na mambo ambayo ungepeta yasipitishwe,” akaongeza.

Hata hivyo, Naibu Rais amekiri kukubaliana na baadhi ya maswala yaliyomo kwenye ripoti ya BBI kama vile swala la uchumi kwa Wakenya wa kipato cha chini, kuchaguliwa kwa maseneta 47 wanawake na kuundwa kwa maeneo bunge 70 zaidi.

Haya yanajiri huku shughuli ya ukusanyaji sahihi za BBI ikiwa inaendelea kote nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *