Ruto asitisha mikutano yake ya kisiasa kufuatia ongezeko la maambukizi ya COVID-19

Naibu Rais William Ruto amesitisha mikutano yake ya kisiasa kutokana na hofu ya msambao wa virusi vya Corona.

Kwenye taarifa kupitia mtandao wake wa kijamii, Ruto amesema mikutano iliyokuwa imeratibiwa kufanyika wikendi hii huko Machakos, Kitui na Makueni imeahirishwa.

“Ongezeko la visa vya COVID-19 linaashiria wimbi la pili la maambukizi. Kwa sababu hiyo, nimeamua kupunguza mikutano ya hadhara hadi wakati mwingine,” amesema Ruto.

Uamuzi huo umefanyika siku mbili tu baada ya viongozi wa kidini kumtaka Rais Uhuru Kenyatta kupiga marufuku mikutano yote ya kisiasa kwa vile inavyoathiri vita dhidi ya maambukizi ya Corona.

Jumatatu, Ruto alifanya mkutano na wasomi wa jamii ya Wakamba kutoka kaunti za Makuani, Machakos na Kitui huko Karen, Nairobi.

Naibu wa Rais amekuwa na misururu ya mikutano ya kisiasa kote nchini huku akinuia kujipatia umaarufu katika azma yake ya kuwania urais mwaka wa 2022.

Kwenye mikutano hiyo, Ruto pia amekuwa akitoa hisia zake kuhusu ripoti ya mpango wa maridhiano ya kitaifa BBI iliyozinduliwa juma lililopita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *