Ruto amtaka Raila kukoma kukosoa serikali ya Jubilee kwenye mikusanyiko ya kisiasa

Naibu Rais Dkt. William Ruto amemtaka kiongozi wa upinzani Raila Odinga kushauriana moja kwa moja na Rais Uhuru Kenyatta kuhusiana na madai yake kwamba serikali ya Jubilee imekosa kutimiza ahadi zake kwa Wakenya.

Ruto, aliyekuwa akiongea katika eneo la Dagoretti, amesema inasikitisha kwa Odinga kumkosoa Rais Kenyatta kupitia kwa mikusanyijko ya kisisa ya kando ya barabara na hali amehusika pakubwa katika kuvuruga mipango ya maendeleo ya utawala wa Jubilee kupitia kwa mpango wake wa maridhiano wa mwaka wa 2018.

Naibu Rais amesema kwamba Odinga alibadili malengo muhimu ya utawala wa Jubilee, kwa kushughulikia haswa marekebisho ya katiba badala ya kubuni nafasi za ajira kwa vijana wa humu nchini.

Amesema kinara huyo wa chama cha ODM anapaswa kukubali kwamba yeye ni sehemu ya juhudi zilizokosa ufanisi za kutimiza ahadi anazozungumzia.

“Kama uko na shida na utendakazi wa serikali ya Jubilee, mtafute Uhuru Kenyatta kwa simu ama umtembelee afisini umwambie kwamba kuna shida katika utendakazi wa serikali ya Jubilee,” amesema Ruto.

Wakati uo huo, Dkt. Ruto amesema mpango wa ‘Hasla’ haunuii kuleta migawanyiko kuambatana na tabaka za watu, bali unalenga kuwapa uwezo wale wasiobahatika katika jamii.

Viongozi walioandamana naye waliukosoa mpango wa maridhiano wa BBI na kusema umevuruga ajenda kuu nne za maendeleo ya utawala wa Jubilee.

Wamewataka wale wanaounga mkono mpango wa BBI kuelekeza juhudi zao katika kuwapatia Wakenya uwezo wa kiuchumi badala ya kuendeleza tamaa zao za kisiasa.

Hivi majuzi, Odinga alisema utawala wa Jubilee umeshindwa kutimiza ahadi zake za kabla ya uchaguzi, hususan mradi wa vipakatalishi kama ilivyoahidiwa mwaka wa 2013.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *