Ruto akosoa ufufuzi wa kesi za ghasia za baada ya uchaguzi

Naibu Rais Dkt. William Ruto amesema ufufuzi wa kesi za ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 unaweza kusababisha chuki za kikabila na migawanyiko.

Ruto, kupitia mtandao wake wa kijamii wa Twitter, amesema ufufuzi wa kesi hizo ni jaribio lenye nia mbaya la kufufua hisia za kikabila.

Amesema hisia hizo ziliangamizwa kwa utambuzi wa vuguvugu la Hustler kwamba umaskini na ukosefu wa ajira ambao umesababishwa na uongozi duni ndio tatizo kubwa, wala sio makabila ya humu nchini.

Matamshi ya Ruto yanajiri baada ya kuripotiwa hapo awali kwamba kesi za ghasia za baada ya uchaguzi mwaka wa 2007 na 2008 zitafunguliwa tena, huku waathiriwa wakiwa tayari kutoa ushahidi.

Idara ya Upelelezi wa Jinai hata hivyo imefafanua kwamba haina nia ya kufungua tena kesi zilizohitimishwa bali ni kesi mpya zilizoripotiwa na waathiriwa.

Kwenye taarifa kwa wanahabari iliyotiwa saini na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi George Kinoti, idara hiyo imesema haiwezi kufungua tena kesi ambayo tayari imeamuliwa mahakamani kwani hatua hii inaweza kuwa na madhara mara dufu kama inavyofafanuliwa kwenye katiba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *