Ronaldinho sasa ni mwanamuziki

Ronaldo De Assis Moreira maarufu kama Ronaldinho Gaucho ni mcheza soka mstaafu maarufu sana ulimwenguni mzaliwa wa Brazil. Ronaldinho anaonekana kuingilia muziki sasa miezi kadhaa baada ya kuachiliwa huru kutoka gerezani.

Haya yamedhihirika wazi baada yake kuonekena kwenye video ya wimbo wa mwanamuziki Tropa Do Bruxo unaoitwa “Rolê Aleatório” ambapo anaimba akiwa amezingirwa na kina dada.

Duru zinaarifu kuwa mwaka huu wa 2021 Ronaldinho anapania kuzindua vibao vinane. Yeye na kakake walitiwa mbaroni wakati fulani mwaka jana kwa kile kilichosemekana kuwa kujaribu kuingia Paraguay na stakabadhi za uongo.

Waliachiliwa mwezi wa nne mwaka jana baada ya siku 32 tu na walikuwa wamehukumiwa kifungo cha miezi sita gerezani lakini hajasema iwapo muda wake gerezani ulichochea aingilie muziki.

Sio mara ya kwanza mchezaji huyo wa awali wa Barcelona kutunga na kuimba wimbo, mara ya kwanza aliunda wimbo ni mwaka 2016 ambao ulitumiwa kama wimbo rasmi na wanaspoti walemavu huko Rio.

Mwaka 2017 alizindua kibao kingine kwa jina “Sozinho” maana yake “Peke yangu” au “Alone” kwa kiingereza na mwaka 2019 akafanya wimbo mwingine wa siasa miezi kadhaa baada ya magari yake kutwaliwa.

Alipohijiwa, Ronaldinho alisema amependa muziki tangu zamani na ni wakati sasa aingilie akipendacho.

Ronaldinho wa miaka 40 sasa, anatumai muziki wake utagusa nyoyo za watu moja kwa moja. Wakati akisakata soka, Ronaldinho alijishindia tuzo kadhaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *