Roma Zimbabwe azomea wanamuziki wenza

Mwanamuziki wa Tanzania Ibrahim Mussa maarufu kama Roma Mkatoliki au Roma Zimbabwe amejitokeza na kuzomea wanamuziki wenza hasa waanzilishi wa muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania.

Alifanya hivyo kupitia video ambayo alipachika kwenye akaunti yake ya Instagram na anaanza kwa kuomba radhi kwani huenda akakera wengine.

Kulingana naye, wanamuziki hao wa zamani wamekuwa wakilalamika kwamba hawapatiwi nafasi na waandalizi wa tamasha lakini amegundua wanajiponza wenyewe.

Mwanamuziki huyo alivaa viatu vya shabiki mpenda muziki na kusema kwamba wanamuziki ambao walianza kazi kabla ya mwaka 2005 wanapoingia jukwaani sasa hawawezi kutumbuiza kabisa. Anasema wengi hawatii bidii kukumbuka maneno ya nyimbo zao na wanapokuwa jukwaani wanajisahau wanaanza kuhimiza umati uinue mikono juu na mambo kama hayo.

Roma ambaye mwaka jana mwezi Disemba alitangaza kwamba anaacha kazi ya muziki, anashindwa kuelewa ni kwa nini msanii hawezi kutumia muda kujitayarisha kwa ajili ya kutumbiuza ilhali alijua mapema kuhusu tamasha. Kwa maoni yake, hiyo ndiyo sababu kuu ya waandalizi wa tamasha kuwasusia maanake hawaridhishi hata wanapopata fursa.

Lengo la ukosoaji wake anasema ni kuamsha wanamuziki kama hao ili wadumishe heshima na hadhi yao katika ulingo wa muziki nchini Tanzania.

Mkali huyo wa muziki wa kufokafoka ambaye alihamia nchini Marekani alitoa mfano wa wanamuziki wa Marekani wakongwe ambao huridhisha sana wanapoingia jukwaani hata baada ya miaka mingi kama vile Snoop Dog.

Alizungumzia pia mwanamuziki wa Tanzania marehemu Mangwea ambaye anasema alikuwa mzuri sana kwa kazi ya kutumbuiza moja kwa moja na hakutegemea kuchezewa kanda iliyorekodiwa. Lakini analalamika kwamba kazi zake hazipatikani mitandaoni kwa ajili ya kumbukumbu.

Roma anamtaja pia marehemu Ruge mutabaha ambaye alikuwa mwandalizi mkubwa wa tamasha na mwekezaji katika sekta ya vyombo vya habari ambaye alikuwa akihakikisha kila aliyempa nafasi ya kutumbuiza kwenye tukio lake amefanya mazoezi kabla ya siku hiyo huku akiwasaidia kupanga kazi zao jukwaani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *