Roma Zimbabwe aomba kura za MAMA

Mwanamuziki wa Tanzania ambaye kwa sasa yuko Marekani Roma Zimbabwe au ukipenda Roma Mkatoliki ameomba watazania kura.

Kundi lake na mwanamuziki mwenza Stamina kwa jina “Rostam” limeteuliwa kuwania tuzo la kundi bora la mwaka chini ta tuzo za Mtv Africa Music Awards – MAMA ambazo zitaandaliwa nchini Uganda mwakani.

Kwenye akaunti yake ya Instagram, Roma aliweka video fupi ya kibao chao na kuandika, “Wasanii wa Hip hop Bongo tulisemwa na tukasimangwa sana kuwa hatuingii kwenye tuzo za kimataifa!! Wanaingia tu Kenya, Nigeria na Afrika Kusini kila wakati. Haya leo vijana wenu Rostam wameingia. Ile nguvu mliyokuwa mnatumia kuwasema wana hip hop, ihamishie kwenye kupiga kura tuzo lije nyumbani.”

Anaendelea kwa kuwaelekeza mashabiki kuhusu namna ya kupiga kura akiiwahimiza wapige kura nyingi wawezavyo.

Haya yanajiri siku chache baada ya Roma kutangaza kwamba anang’atuka kwenye ulingo wa muziki baada ya miaka 13.

Aliachia video ya wimbo ambao amemshirikisha Lady Jaydee kwa jina “Diaspora” ambao alisema ndio wimbo wake wa mwisho.

Hata hivyo Stamina alisema kwamba watu walitafsiri visivyo maneno ya Roma Mkatoliki. Kulingana naye, Roma alisema anaachia wimbo wake wa mwisho na wala hakusema anaacha muziki.

Stamina alisema pia kwamba kundi la Rostam litaendelea kama kawaida ingawa kila mmoja ana meneja tofauti.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *