Categories
Habari

Ripoti ya BBI kuzinduliwa rasmi leo

Ripoti ya mpango wa maridhiano ya kitaifa BBI iliyosubiriwa kwa muda mrefu inatarajiwa kuzinduliwa rasmi leo.

Hafla ya uzinduzi wa ripoti hiyo kwa umma itaongozwa na Rais Uhuru Kenyatta katika Ukumbi wa Bomas, Jijini Nairobi.

Haya yanajiri baada ya Rais Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga kukabidhiwa ripoti hiyo huko Kisii, Jumatano.

Siku hiyo, Rais aliwahimiza Wakenya kuisoma ripoti hiyo na kuyaelewa vyema yaliyo ndani yake badala ya kupotoshwa na wanasiasa.

Alisema lengo kuu la BBI ni kuleta utangamano wa kitaifa, usawa wa wananchi na maendeleo ya nchi, akihoji kwamba mchakato wa mpango huo uko wazi kwa Wakenya wote.

Kenyatta aliwaonya viongozi dhidi ya kuingiza siasa katika swala la ripoti hiyo na kuleta mashindano na badala yake washirikiane ili kuboresha yaliyomo kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Naye kinara wa ODM Raila Odinga alisema kuwa BBI italeta suluhu ya changamoto nyingi zinazolikumba taifa hili kama ufisadi, italeta maridhiano, umoja wa kitaifa, nafasi za kujiendeleza kwa wote na usalama nchini.

Wadau wa sekta mbali mbali pia wametaka kujumuishwa kwa kila mmoja kwenye mdahalo huo wa BBI unaotarajiwa kuwa ajenda kuu katika majuma machache yajayo baada ya rais kuzindua rasmi ripoti hiyo.

Tayari ripoti hiyo imezua hisia mseto miongoni mwa viongozi na Wakenya kwa jumla, huku wengine wakiiunga mkono na wengine wakiipinga kwa kusema kuwa haitasuluhisha matatizo ya wananchi bali itawafaidi wakuu wa serikalini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *