Redio inayoongozwa na wanawake Afrika Kusini

Mwanamuziki wa muda mrefu nchini Afrika Kusini Yvonne Chaka Chaka alifungua kituo cha redio cha mitandaoni ambacho kinaendeshwa na wanawake.

Stesheni hiyo kwa jina “WOMan Radio” imekuwa wazo la mwanamuziki huyo ambaye pia ni mwigizaji kwa muda mrefu. Mwaka 2016 ndio kwanza alifikiria hilo lakini akaliweka kando kidogo kwani anasema data ya kuingia kwenye mitandao ya kijamii ni ghali nchini Afrika kusini.

Yvonne akiwa mbele ya bango la Kituo chake cha Redio

Anasema alitiwa moyo na waziri wa mawasiliano nchini Afrika Kusini Bi. Stella Thembisile ambaye alimkumbusha kwamba yeye ana ufuasi hata nje ya Afrika kusini.

Yvonne anasema alichochewa sana na hitaji la kuwapa kina dada uwezo na wakiwa wanaweza kujisimamia itakuwa rahisi pia kwa wanaume kuhusiana nao.

Kulingana naye kituo hicho kinatoa nafasi kwa kina dada kusimulia hadithi zao ili kuwatia moyo wanawake wengine, kuwapa ushauri, mafunzo na hata mawazo ya biashara.

Mwimbaji huyo wa wimbo “Umqombothi” anasema kuna wanawake ambao wanadhulumiwa kwenye ndoa au mahusiano na hawajui na kituo hicho kitawafungua macho watu kama hao.

Alifafanua kwamba kituo hicho ambacho kilianza rasmi mwezi Oktoba hakikuundwa kwa sababu ya kudhalilisha wanaume.

Kitahusisha pia wanawake kutoka nchi mbali mbali barani Afrika na alitaja nchi kama vile Kenya na Uganda ila kwa sasa watangazaji wote ni raia wa Afrika Kusini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *