Miamba wa soka nchini Misri Zamalek walijiweka katika nafasi nzuri ya kutinga fainali ya kipute cha ligi ya mabingwa Africa Caf baada ya kukosa heshima za mgeni na kuwaadhibu Raja Casablanca ya Moroko bao 1-0 katika duru ya kwanza ya semi fainali Jumapili usiku.
Katika mchuano huo uliopeperushwa mbashara na runinga ya Kbc ulishuhudia wenyeji Casablanca wakitawala mechi kwa kipindi kirefu lakini wakakosa kumakinika mbele ya lango la Zamalek.
Achraf Bencharki ambaye ni raia wa Moroko alirejea nyumbani katika uwanja wa Complex Mohammed V na kuwafungia Zamalek bao la pekee na la ushindi kunako dakika ya 18 kipindi cha kwanza kwa njia ya kichwa .
Zamalek walicheza mchezo wa kujihami katika kipindi cha pili chote na kunusurika kwa ushindi huo maridhawa.
Mkondo wa pili utachezwa katika uwanja wa kimataifa wa Cairo Jumamosi hii .
Timu za Misri zilisajili matokeo mazuri ugenini nchini Moroko huku pia mabingwa mara 8 Al Ahly pia walikuwa wamewashinda Wydad Casablanca ya Moroko Jumamosi iliyopita mjni Casablanca na watapiga mechi ya marudio Jumapili hii.