Rais wa Somaliland atua Kenya kwa mashauriano na Rais Kenyatta

Rais wa eneo la Somaliland, Musa Bihi Abdi amewasili humu nchini leo alasiri na kulakiwa na Waziri wa Kilimo Peter Munya na Katibu Mkuu Mwandamizi katika Wizara ya Mashauri ya Nchi za Kigeni Ababu Namwamba.

Taarifa kwenye mtandao wa kijamii wa Wizara ya mashauri ya nchi za kigeni imedokeza kwamba Rais Abdi anatarajiwa kushauriana na Rais Uhuru Kenyatta Jumatatu.

Wizara hiyo pia imesema kuwa Kenya haina uwakilishi wa kidiplomasia huko Somaliland lakini inatambua uthabiti wa kisiasa na kiuchumi wa eneo hilo na inaazimia kuimarisha biashara katika bidhaa na huduma na pia uwekezaji kama nguzo ya ushirikiano wa kimaendeleo wa kudumu katika kanda hii.

Hii ni ziara ya pili ya kiongozi huyo wa Somaliland baada ya ziara sawa na hiyo ya Rais Kahin Riyale Kahin mwaka wa 2006.

Somaliland ni mshirika muhimu katika eneo la upembe wa Afrika katika vita dhidi ya ugaidi na hasa kundi la Al-Shabaab.

Somaliland ilitangaza uhuru wake baada ya kung’atuliwa kwa aliyekuwa Rais wa Somalia Siad Barre mwaka wa 1991.

Hatua hiyo ilifuatia juhudi za kujitenga ambapo vikosi vya Siad Barre viliwasaka wapiganaji waasi katika eneo hilo.

Maelfu ya watu waliuawa huku miji ikiharibiwa.

Ingawa haitambuliki, Somaliland ina mfumo wa kisiasa, taasisi za kiserikali, idara ya polisi na sarafu zake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *