Rais wa Afrika Kusini ajitenga baada ya mtu waliyekutana kupatikana na Corona

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amejitenga baada ya mgeni aliyetangamana naye Jumamosi kupatikana na virus vya Corona.

Kulingana na taarifa kutoka afisi ya rais nchini humo, Rais Ramaphosa hajaonyesha dalili zozote za ugonjwa wa COVID-19 na atapimwa iwapo ataanza kuonyesha dalili hizo.

Siku ya Jumamosi, rais huyo alihudhuria hafla ya kuchangisha pesa iliyoandaliwa na Wakfu wa Adopt-a-School, ilihudhuriwa na jumla ya wageni 35 katika hoteli moja mjini Johannesburg.

Jumapili, mmoja kati ya wageni waliohudhuria hafla hiyo alionyesha dalili za ugonjwa huo, akapimwa Jumatatu na Jumanne akapokea matokeo ya kuonyesha kuwa ameambukizwa virusi hivyo.

Wageni wote waliohudhuria hafla hiyo walifahamishwa kuhusu kisa hicho jana na wakalazimika kujitenga, akiwemo Rais Ramaphosa.

Kulingana na taarifa hiyo kutoka afisi ya rais, kanuni za kuzuia mamabukizi ya virusi vya Corona zilizingatiwa kikamilifu kwenye hafla hiyo.

“Hafla hiyo ilizingatia kanuni za COVID-19 ikiwemo uchunguzi wa joto la mwilini, wageni kukaa mbali mbali na uvaaji wa barakoa. Kama wageni wengine wote, Rais alivua barakoa wakati wa chakula na alipokuwa akihutubia wageni tu,” inaeleza taarifa hiyo.

Rais huyo ametuma jumbe za kheri kwa mgeni aliyepatikana na virusi hivyo ambaye anapokea matibabu, akimuombea uponyaji wa haraka na pia kuwatakia wageni wengine afya njema.

Ramaphosa ataendelea kutekeleza majukumu yake kutoka mahali alipojitenga na atazingatia muongozo wa kuhusu karantini kikamilifu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *