Rais Uhuru Kenyatta akabidhiwa ripoti ya BBI

Ripoti iliyosubiriwa kwa hamu ya BBI hatimaye imewasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga.

Akipokea ripoti hiyo, Rais Kenyatta aliwahimiza Wakenya kusoma na kuelewa yaliyomo kwenye ripoti hiyo ili kufanya uamuzi ufaao bila ushawishi wa kisiasa.

Aidha alitangaza kwamba kongamano litaandaliwa kwenye ukumbi wa Bomas siku ya Jumatatu ijayo ambapo jopo hilo litafafanua zaidi yaliyomo kwenye ripoti hiyo.

”Huu si wakati wa migawanyiko ya kisiasa, huu ni wakati wa kuonyesha uongozi na kuunganisha taifa hili pamoja. Siku ya Jumatatu katika ukumbi wa Bomas tutasoma ripoti hii mstari baada ya mwigine. Kabla ya jumatatu ripoti hii inapaswa kusambaziwa wakenya wote,” alisema rais.

Rais alisema marekebisho ya kikatiba yanayopendekezwa yanalenga kuleta mabadiliko ya kina ya kisiasa na kiuchumi humu nchini.

Kiongozi wa taifa aliwataka wanasiasa kukoma kuingiza siasa kuhusu ripoti hiyo badala yake aliwataka kuboresha yaliyomo kwenye ripoti hiyo.

“Tusipoteze fursa hii kupitia tofauti zetu za kisiasa. Tunaweza dhibiti maazimio yetu kwa manufaa ya taifa hili,” alisema rais.

Rais alilishukuru jopo kazi lililoandaa ripoti hiyo kwa kuangazia masuala muhimu yanayowakumba Wakenya.

Rais alilitaka jopo hilo kuhakikisha ripoti hiyo inasambazwa kwa Wakenya kwa kutumia vyombo vya habari ili kuhakikisha wataisoma na kuielewa.

Kwa upande wake kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga alisema ripoti hiyo inajumuisha maoni ya wakenya akidokeza kuwa inashughulikia maswala yaliyodumaza taifa hili kwa miaka mingi.

“Ripoti hii si ya kumfanya Raila awe rais au Uhuru Kenyatta kuwa waziri mkuu. Haya tu ni mapendekezo . Tutakusanya sahihi kupeleka kwa tume ya uchaguzi IEBC na pia kwa mabunge ya kaunti,” alisema Raila.

Kamati ya BBI ya wanachama 14 imekuwa ikishughulikia mabadiliko ya kisheria,Sera,katiba na pia ya kiutawala.

Kabla ya kuandaliwa kwa kura ya maamuzi,jopo hilo la BBI linapaswa kukusanya sahihi milioni moja na kuwasilisha kwa tume ya uchaguzi nchini kuidhinishwa kisha kwa mabunge ya kaunti.

Iwapo ripoti hiyo itaungwa mkono na mabunge ya kaunti 25, itawasilishwa katika bunge la kitaifa ili kuandaliwa kwa mswada wa kura ya maamuzi.

 

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *