Rais Lazarus Chakwera akiri kuchangia msambao wa COVID-19 Malawi

Rais wa Malawi Lazarus Chakwera amekubali lawama baada ya kuorodheswha miongoni mwa waliochangia msambao wa ugonjwa wa COVID-19 nchini mwake mnamo siku za hivi punde.

Rais huyo alishtumiwa vikali juma lililopita baada ya picha za video kusambazwa mitandaoni, zikimuonyesha yeye na mwana-muziki mashuhuri aliyekuwa ziarani nchini Malawi, Madonna.

Wawili hao walionekana wakiamkuana na kupigwa picha wakiwa pamoja bila kuvalia barakoa wala kudumisha umbali unaohitajika baina ya watu.

Malawi imeshuhudia ongezeko kubwa la visa vya COVID-19 mnamo wiki za hivi punde, huku watu kadhaa mashuhuri, akiwemo muimbaji na mtangazaji Maria Chidjanja Nkhoma na pia Mkuu wa Masuala ya Utawala katika Wizara ya Habari Ernest Kantchentche, wakiwa miongoni mwa waliofariki kutokana na ugonjwa huo.

Zaidi ya raia 200 wa Malawi wameripotiwa kufariki kufikia sasa kutokana na ugonjwa wa COVID-19, huku 30 kati yao wakifariki katika muda wa wiki mbili zilizopita pekee.

Rais Chakwera, ambaye pia ni kasisi, amesema ataanza kipindi cha siku 21 za kufunga na kumwomba Mwenyezi Mungu kuiponya nchi yake.

Aidha, Chakwera amewaagiza maafisa wa usalama kufanikisha utekelezaji wa hatua mpya za kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na kufungwa kwa bar na vilabu vya usiku itimiapo saa mbili usiku.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *