Rais Kenyatta, viongozi wengine waifariji familia ya Mudavadi kufuatia kifo cha Mama Hannah Mudavadi

Rais Uhuru Kenyatta ametuma risala ya rambi rambi na faraja kwa familia ya Mudavadi kufuatia kifo cha mama Hannah Atsianzale Mudavadi.

Mama Hannah aliyekuwa na umri wa miaka 92 alikuwa mjane wa Waziri wa zamani marehemu Moses Mudamba Mudavadi na mamake kinara wa chama cha ANC, Wycliffe Musalia Mudavadi.

Kwenye rsala yake, Rais Kenyatta amemtaja mama Hannah kuwa mkarimu na mnyenyekevu aliyedumisha maadili ya familia na kuchangia pakubwa katika ustawi wa jamii.

Rais Kenyatta amesema mama Hannah atakumbukwa kwa wajibu wake wa kufanikisha elimu kwa kuwasaidia wanafunzi kutoka familia zisizojiweza kupata masomo.

Rais amemliwaza Musalia Mudavadi na familia nzima na kuitakia faraja wakati huu wa majonzi.

Kwenye ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, chama cha ANC kimetangaza kuwa mama Hannah amefariki Jumatatu saa kumi na moja asubuhi katika Hospitali ya Nairobi.

Wakati uo huo, Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga pia wametuma risala za rambi rambi kwa familia hiyo.

Kwenye rambi rambi yake, Ruto amemtaja mama Hanna kuwa mcha Mungu na mwanamke mwenye heshima, aliyewajibika, ambaye aliwalea vyema wanawe.

Naye kinara wa chama cha ODM Raila Odinga amesema alipokea habari za kifo cha Mama Hannah Atsianzale Mudavadi kwa huzuni nyingi.

Akimfariji Musalia Mudavadi na familia yake, Raila amemuomba Mwenyezi Mungu aipe nguvu familia ya Mudavadi wakati huu mgumu wa maombolezo.

Risala nyingine zimetumwa na kiongozi wa chama cha KANU Gideon Moi, ambaye amemtaja mama Hannah kuwa mnyenyekevu, mcha Mungu na mama aliyejali maslahi ya wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *