Rais Kenyatta ndiye mwenyekiti mpya wa Jumuia ya Afrika Mashariki

Rais Uhuru Kenyatta amejitolea kuhakikisha kuwa jumuiya ya Afrika mashariki inaungana na kustawi zaidi, baada ya kutwaa uenyekiti wa jumuiya hiyo.

Rais alisema kuwa atahakikisha kuwa maazimio ya pamoja ambayo yalizalisha muungano huo miaka 20 iliyopita, yanatimia.

Rais Kenyatta ambaye alikuwa akihutubia kongamano la 21 la kawaida la viongozi wa jumuiya ya Afrika mashariki, lililoandaliwa kupitia kwa mtandao kutokana na janga la virusi vya corona, baada ya kutwaa wenyekiti kutoka kwa rais wa Rwanda Paul Kagame, alimpongeza hayati rais mstaafu Daniel Arap Moi na hayati rais mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa, huku akitambua majukumu waliyotekeleza pamoja na rais Yoweri Museveni wa Uganda, katika kubuni muungano wa Afrika mashariki miaka 20 iliyopita.

Rais Kenyatta alitumia fursa hiyo kuorodhesha ruwaza yake kwa kanda hii, na kuhakikisha utekelezaji wa miradi na mipango katika sekta za uzalishaji.

Kenya iliondoa sharti la kuwa na visa kwa raia wa Sudan Kusini wanaozuru humu nchini.

Wakati wa mkutano huo, Dkt Peter Mutuku Mathuki wa humu nchini aliapishwa kuwa katibu mkuu mpya wa jumuia ya Afrika Mashariki.

Dkt. Mathuki atahudumu kwa muhula mmoja wa miaka mitano kuanzia tarehe 25 mwezi April mwaka 2021.

Dkt. Mathuki amechukua wadhifa huo kutoka kwa balozi Libérat Mfumukeko wa  Burundi ambaye muhula wake unakamilika

Mkutano huo chini ya uenyekiti wa Rais Uhuru Kenyatta, ulishuhudia kuapishwa kwa majaji  sita wapya wa Mahakama ya haki ya Afrika ya Mashariki akiwemo mkenya Kathurima M’inoti ambaye anajiunga na kitengo cha rufaa cha Mahakama hiyo ya haki ya Afrika  mashariki.

Akizungumza alipomkabidhi wadhifa huo Rais Uhuru Kenyatta, Rais Paul Kagame alimpongeza Rais Kenyatta anapotwaa haramu za uenyekiti wa jumuia ya Afrika Mashariki na pia akamkaribisha Dkt. Mathuki  katika wadhifa wa katibu mkuu wa jumuia ya Afrika ya mashariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *