Rais Kenyatta kutoa hotuba ya 2020 kuhusu hali ya taifa Juma lijalo

Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kutoa hotuba ya mwaka huu kuhusu hali ya taifa hili kwenye kikao cha pamoja cha Bunge la Seneti na lile la Kitaifa tarehe 12 mwezi huu.

Kwenye arifa yake kwa Bunge la Kitaifa jana, Spika Justin Muturi alisema mkutano huo utafanywa kwa kuzingatia maagizo na kanuni za Wizara ya Afya.

“Nataka kujulisha Bunge kwamba nimepokea ujumbe kutoka kwa Rais, uliochapishwa tarehe 23 Oktoba, 2020, kwamba ananuia kutoa hotuba ya 2020 kuhusu hali ya taifa Bungeni siku ya Alhamisi tarehe 12 Novemba, 2020,” akasema Spika Muturi.

Hotuba hiyo ya kila mwaka inatolewa kwa mujibu wa katiba na inaangazia maendeleo ya taifa na hatua ambazo zimechukuliwa kuafikia maadili ya kitaifa.

Ripoti ya mpango wa maridhiano ya kitaifa, BBI na ajenda nne kuu za maendeleo za Rais ni miongoni mwa mambo ambayo yanatarajiwa kuangaziwa kwenye hotuba hiyo kwa taifa.

Wakati uo huo, Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa  kufanya kikao maalum na magavana leo ili kuafikiana kuhusu hatua zitakazochukuliwa kukabiliana na wimbi la pili la chamko la ugonjwa wa COVID-19.

Haya yanajiri kutokana na hofu kwamba huenda sheria mpya zikatangazwa na hata shughuli kufungwa ili kudhibiti msambao wa virusi vya Corona humu nchini.

Jana Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Wycliffe Oparanya alisema kaunti sasa zimesakamwa na visa vya maambukizi ya ugonjwa huo, huku zikiripoti visa vingi vipya vya maambukizi kuliko ilivyokuwa hapo nyuma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *