Rais Kenyatta awataka viongozi wapunguze joto la siasa

Rais Uhuru Kenyatta amewataka viongozi wa kisiasa wapunguze kasi ya siasa za mwaka wa 2022 na badala yake watilie mkazo juhudi za kuunganisha Wakenya.

Kwenye ujumbe wake wa moja kwa moja kwa Naibu Rais William Ruto, Rais amesema, japo kwa utani, kwamba Ruto amepoteza dira baada ya kuonekana kuangazia zaidi kampeni za urais katika uchaguzi mkuu ujao.

“Namshukuru Naibu Rais, tumetembea pamoja hadi wakati siasa za 2022 zilipomfanya asahau kila kitu. Watu wanafaa kuwa watulivu kwanza, wakati huo utafika,” amesema Rais.

Amesema hayo kwenye hotuba yake katika hafla ya kuzindua rasmi ripoti ya BBI kwa umma iliyofanyika katika Ukumbi wa Bomas, Jijini Nairobi.

Rais Kenyatta amefananisha hali hiyo na mbio za kupokezana ambapo ameuchekesha umati kwa kusema kuwa badala ya kuendeleza mbio hizo, naibu wake amegeuka na kukimbia akirudi nyuma.

Rais pia ameeleza kuwa alitaka kutumia siku hiyo kumshukuru Ruto, akihoji kuwa amekuwa akimhusisha katika mchakato wa maridhiano na kinara wa ODM Raila Odinga.

“Nataka pia nimshukuru Naibu Rais, katika mchakato huu nimekuwa nikimueleza yaliyokuwa yakiendelea. Amekuwa sehemu ya mchakato huo, huu ni ukweli siwadanganyi, mnaweza kumwuliza yupo hapa. Kwanza alinisaidia kuchagua baadhi ya wazee amabao nimewataja hapa,” akasema kiongozi wa taifa.

Aidha, Rais Kenyatta amemsifu Raila kwa ukarimu wake na kulenga maridhiano, akisema kuwa hakutaka kupewa sehemu ya uongozi serikalini.

Ameongeza kuwa maridhiano yake na Raila yaliyozalisha BBI hayalengi kujipatia nafasi serikalini bali walikuja pamoja kwa lengo la kusitisha mapigano ambayo yamekuwa yakishuhudiwa humu nchini baada ya kila uchaguzi tangu mwaka wa 1992.

Kenyatta amekuwa wazi kwamba wanataka kuleta kila mtu kwenye mchakato huo ili kuhakikisha kwamba hakuna mkenya anayeachwa nyuma.

Amesema wataendelea kushauriana na viongozi mbali mbali akihoji kuwa kama taifa, Wakenya wanaweza kuiboresha ripoti ya BBI, akiwataka walio na maoni kuhusu ripoti hiyo wayalete mezani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *