Rais Kenyatta awahimiza vijana wachangamkie maswala ya kitaifa

Rais Uhuru Kenyatta ametoa wito kwa vijana kushiriki ipasavyo katika maswala muhimu ya kitaifa.

Rais Kenyatta amesema kuwa wakati umewadia kwa vijana kuchukua ushukani wa maswala ya humu nchini.

Rais amesema kuwa licha ya vijana kuwa zaidi ya asilimia 70 ya idadi ya Wakenya, hawajashiriki ipasavyo katika uongozi wa taifa hili.

Kiongozi wa taifa amesema hayo katika ukumbi wa Bomas, Jijini Nairobi wakati alipozindua rasmi mjadala wa kitaifa wa vijana kwa jina ‘Kenya ni Mimi’.

Rais ameongeza kuwa vijana wanahitaji kutumia idadi yao kuwania nyadhifa za uongozi nchini.

Amekariri kwamba vijana lazima wawe katika msitari wa mbele kuboresha maisha yao na taifa hili kwa jumla.

“Lazima muwe ndani ya uwanja wala sin je ya uwanja. Lazima mshiriki katika mjadala wa nchi hii kama mtaamua kwamba mnataka kushika usukani wa hatma ya nchi. Mko na nafasi kubwa,” amesema Rais.

Kuhusu mizozo ya kijinsia na tamaduni nyingine zilizopitwa na wakati kama vile ukeketaji na ndoa za mapema, Rais Kenyatta amewahakikishia vijana kuwa serikali haitalegeza juhudi za kukabiliana na maovu hayo.

Aliongeza kwamba serikali yake itaendelea kushirikiana kwa karibu na wanawake pamoja na vijana katika nyanja zote za kimaendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *